HOTUBA YA MHESHIMIWA BARAKA LUVANDA, BALOZI WA TANZANIA NCHINI JAPAN, WAKATI WA MAADHIMISHO YA SIKU YA KISWAHILI DUNIANI NA HAFLA YA KUFUNGA WIKI YA EXPO YA UTAMADUNI NA KISWAHILI, OSAKA, JAPAN, TAREHE 7 JULAI 2025
Mheshimiwa Balozi Yasushi Misawa,
Mwakilishi Maalum wa Serikali ya Japan katika Maonesho ya Dunia ya OSAKA 2025,
M(Wa)wakilishi wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO),
Wawakilishi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ya Tanzania,
Wawakilishi kutoka Baraza la Kiswahili Tanzania -(BAKITA na BAKIZA)
Viongozi na wawakilishi wa taasisi mbalimbali, wanataaluma, wanafunzi na wadau wa Kiswahili,
Wageni waalikwa,
Mabibi na Mabwana.
Habari za Asubuhi?
Mina san Ohayo Gozaimasu!
Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuwezesha kukutana hapa siku hii ya leo.
Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, na kwa nafasi yangu binafsi, ninapenda kutoa salamu za dhati za pongezi na shukrani kwa kila mmoja wenu kwa kuhudhuria Maadhimisho haya ya Siku ya Kiswahili Duniani.
Tofauti na miaka iliyopita, mwaka huu tuliamua kuiadhimisha siku hii maalum ndani ya viunga vya Maonesho ya Dunia ya OSAKA 2025 yanayoendelea mahali hapa.
Maadhimisho haya ni ya Siku ya Kiswahili Duniani ni ya kihistoria kwani yanadhihirisha hadhi ya Kiswahili kama lugha ya kimataifa.
Lugha hii imedhihirika kuwa na mchango mkubwa si tu katika kuunganisha jamii za Watanzania au wana-Afrika Mashariki, bali pia kuwa jukwaa la kukuza diplomasia, biashara, utalii, na maendeleo ya kielimu duniani kote na zaidi, kukuza amani na maelewano miongoni mwa jamii zinazotumia lugha hii adhimu.
Napenda kurejea kuishukuru sana UNESCO kwa kutambua mchango mkubwa wa Kiswahili katika kudumisha utofauti wa tamaduni (cultural diversity), kudumisha ufahamu na mawasiliano miongoni mwa jamii za waliostaarabika na mawasiliano na umoja miongoni mwa jamii tofauti duniani. Hivyo, kwa kutambua mchango huo mkubwa UNESCO kupitia Azimio Namba 41 C/61 la Mwaka 2021 lilitangaza tarehe 7 ya mwezi Julai kila mwaka kuwa Siku ya Kiswahili Duniani. Tukio hili ni fahari kubwa siyo tu kwa Tanzania bali pia kwa watumiaji wote wa Kiswahili duniani.
Aidha, napenda kuishukuru kwa dhati Serikali ya Japan kwa kushirikiana nasi katika kuenzi lugha hii adhimu kupitia programu mbalimbali za kitaaluma na kiutamaduni. Ushirikiano huu ni kielelezo cha uhusiano madhubuti na imara wa kidiplomasia baina ya nchi hizi mbili.
Mabibi na Mabwana,
Katika kuendeleza dhamira yetu ya kukuza Kiswahili nchini Japan, pamoja na mambo mengine, leo tutashuhudia utiaji saini wa Hati ya Ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na Chuo Kikuu cha Osaka. Ushirikiano huu wa kitaaluma utatoa fursa pana kwa wanafunzi, wahadhiri na watafiti wa pande zote mbili kubadilishana uzoefu na maarifa, kufanya tafiti za pamoja, na kuimarisha mafunzo ya Kiswahili na uelewa wa mila, desturi na tamaduni za pande mbili husika.
Kwa upande mwingine, nipongeze sana taasisi binafsi na za umma ambazo zinafundisha na kuendeleza Kiswahili nchini Japan.
Mchango wenu ni mkubwa na wa kupongezwa. Leo, kwa heshima kubwa, tunatambua na kutoa tuzo kwa taasisi 13 na watu binafsi waliotoa mchango wa kipekee katika kufundisha Kiswahili nchini Japan. Ni matumaini yangu kwamba tuzo hizi zitawatia moyo wa kuendeleza juhudi hizi muhimu.
Tunamini pia kuwa tuzo hizi zitawavutia wengine kujitokeza kufanya kazi hiyo nzuri ya kukuza Kiswahili nchini Japan.
Na kwa hakika Tanzania ina matumaini makubwa kwa ndugu na marafiki wetu wa Japan. Kama nilivyosema awali, Tunatambua na kuthamini juhudi zinazofanywa na vyuo vikuu, vituo vya lugha, wanataaluma na wanafunzi hapa Japan katika kujifunza, kufundisha na kuendeleza lugha ya Kiswahili.
Lakini pia tunayo matarajio kuwa:
i) Kiswahili kitaendelea kuingizwa rasmi katika mitaala ya vyuo vingi zaidi hapa Japan, na kwamba idadi ya wanaojifunza lugha hii itaongezeka kwa kasi;
ii) Ushirikiano baina ya taasisi za elimu ya juu ya Tanzania na Japan utaimarika, hasa kupitia programu za kubadilishana wanafunzi, walimu, na watafiti wa Kiswahili na masuala ya kitamaduni;
iii) Wajapani watazidi kuonesha hamasa ya kutumia Kiswahili si tu kwa lengo la kielimu, bali pia katika biashara, diplomasia, utalii, na mawasiliano ya kimataifa;
iv) Na zaidi ya yote, kwamba Kiswahili kitakuwa kiungo muhimu cha maelewano na urafiki wa kudumu kati ya wananchi wa Tanzania na Japan.
Kwa mnasaba huo, kwa pamoja tutaendelea kujenga daraja la mawasiliano kupitia Lugha adhimu ya Kiswahili – daraja ambalo halina mipaka ya kijiografia, bali lina nguvu ya kuunganisha mioyo na fikra kwa misingi ya heshima, amani na maendeleo ya pamoja.
Mabibi na mabwana,
Naomba mniruhusu kuhitimisha hotuba yangu kwa kutabainisha kuwa Kiswahili ni zaidi ya lugha – kwani ni kiini cha utambulisho wetu kama Waafrika. Kupitia Lugha hii, tunaelezea historia yetu duniani, tunatangaza maliasili na vivutio vyetu, na kuhamasisha dunia kuhusu thamani ya maelewano na mshikamano tulionao kama Taifa.
Nitoe wito wa kuendelea kushirikiana kukuza Kiswahili duniani, hususan, kwa kuwekeza katika tafsiri, fasihi, teknolojia ya lugha na tafiti za kitaaluma. Tunapofanya hivyo, tunalinda urithi wetu na kuileta dunia karibu zaidi kupitia lugha ya amani, upendo na mshikamano.
Asanteni sana kwa kunisikiliza;Mungu Ibariki Tanzania;Mungu Ibariki Japan; Mungu Ibariki Lugha yetu ya Kiswahili.