Tarehe 21 Aprili 2026, Mheshimiwa Anderson Mutatembwa alifanya ziara katika Sophia University kilichopo Tokyo, ambapo alikutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa chuo hicho, Profesa Mariko Iijima.

Katika mazungumzo hayo, Balozi alieleza kuwa madhumuni ya ziara hiyo yalikuwa ni kujitambulisha pamoja na kukishukuru chuo hicho kwa ushirikiano wake mzuri na Sokoine University of Agriculture (SUA). Aidha, alipongeza juhudi za chuo hicho katika kufundisha lugha ya Kiswahili pamoja na ushiriki wake katika maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani mwaka 2025.

Balozi Mutatembwa alitumia fursa hiyo kuomba kuimarishwa zaidi kwa ushirikiano uliopo, ikiwemo kupanua wigo wa ushirikiano kwa kushirikisha vyuo vingine vya Tanzania, hususan vilivyopo Dar es Salaam, Dodoma na Zanzibar. Alisisitiza umuhimu wa kuendeleza ufundishaji wa lugha ya Kiswahili pamoja na kufanya tafiti za pamoja katika masuala ya lugha na utamaduni.

Kwa upande wake, Profesa Iijima alipokea mapendekezo hayo na kuonesha utayari wa Sophia University kuanzisha ushirikiano na vyuo vingine vya Tanzania katika programu za lugha ya Kiswahili. Aidha, alieleza kuwa kuna fursa ya kupanua ushirikiano katika mafunzo ya lugha ya Kijapani kupitia ubadilishanaji wa wahadhiri na wanafunzi, pamoja na kufanya tafiti za pamoja zinazohusu lugha na utamaduni.