Tarehe 20 Aprili 2026, Balozi Anderson Mutatembwa alifanya mazungumzo na Rais wa Tokyo University of Agriculture (Tokyo NODAI), Dkt. Fumio Eguchi, wakati wa ziara yake ya kikazi katika chuo hicho.

Katika mazungumzo hayo, Dkt. Eguchi alieleza shukrani zake za dhati kwa ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tokyo NODAI na Sokoine University of Agriculture (SUA), hususan kufuatia makubaliano ya ushirikiano yaliyosainiwa mwaka 2009. Alibainisha kuwa ushirikiano huo umeendelea kuzaa matunda kupitia programu za kubadilishana wanafunzi, utoaji wa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi kutoka SUA, pamoja na ushiriki endelevu wa wanafunzi hao katika mkutano wa kimataifa wa wanafunzi kuhusu chakula, kilimo na mazingira unaofanyika kila mwaka.

Aidha, Dkt. Eguchi alielezea muhimu wa programu ya Global Agri-Nutrition Leaders Programme katika kukuza wataalamu wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za kimataifa katika sekta ya kilimo na lishe. Alieleza kuwa chuo hicho kimejikita katika dhana ya “Practical Science,” inayolenga kuunganisha nadharia na vitendo katika kujenga ujuzi wa wahitimu.

Kwa upande wake, Balozi Mutatembwa alishukuru kwa ushirikiano huo na kupongeza mchango wa Tokyo NODAI katika kukuza rasilimali watu wa Tanzania kupitia elimu ya kilimo. Alibainisha umuhimu wa kuendeleza na kupanua zaidi ushirikiano huo, hususan katika maeneo ya utafiti, ubunifu na mafunzo ya vitendo yatakayochangia maendeleo ya sekta ya kilimo nchini Tanzania.

Mazungumzo hayo yalihitimishwa kwa pande zote mbili kueleza nia ya kuendeleza ushirikiano huo wa muda mrefu kwa manufaa ya pande zote mbili.