Tarehe 15 Agosti 2023, Ubalozi ulishiriki kwenye uzinduzi wa kahawa ya Tanzania katika Migahawa ya Kahawa ya OBSCURA, iliyopo jijini Tokyo na Hiroshima nchini Japan. OBSCURA ilizindua kahawa aina ya Arabika inayolimwa maeneo ya Iyula na Mahenje, mkoani Songwe; na kahawa aina ya Arabika inayolimwa eneo la Mwika, mkoani Kilimanjaro.
Zoezi hilo la uzinduzi wa kahawa za Tanzania lilienda sambamba na Maadhimisho ya mwezi mzima ya kuitangaza kahawa ya Tanzania nchini Japan, yaliyopewa jina la Tanzania Coffee Trade Fair. Uzinduzi huo ulifanyika kwenye moja ya migahawa yao iliyopo Tokyo na kuhudhuriwa na Mhe. Balozi Baraka Luvanda aliyeambatana na Bi. Edna Dioniz Chuku, Afisa Ubalozi (Masuala ya Uchumi), Bw. Yoshinori Shiba na Hideaki Okamoto, Mtendaji Mkuu na Meneja wa Mauzo wa Migahawa ya OBSCURA, mtawalia.
Aidha, katika uzinduzi huo Balozi Luvanda alipokea maelezo mafupi kuhusu uhusiano wa kibiashara baina ya OBSCURA na wazalishaji wa kahawa wa Tanzania. Bw. Shiba alimweleza Balozi Luvanda kuwa OBSCURA inamiliki migahawa katika miji ya Tokyo na Hiroshima na imekuwa ikijishughulisha na kujipatia umaarufu mkubwa katika ukaangaji wa kahawa (coffee roastering) pamoja na uuzaji wa kahawa iliyo tayari kwa matumizi.
Vilevile, Bw. Shiba alieleza kuwa OBSCURA imekuwa ikijuhusisha na ununuzi wa kahawa ya Tanzania kwa muda mrefu; na huwa wanatembelea mashamba ya kahawa ya Tanzania kila mwaka katika kutafuta masoko mapya ambapo, kwa mwaka hununua wastani wa tani 10 za kahawa ya Tanzania. Alimweleza kuwa mwanzoni mwa mwaka huu, waliweza kutembelea mkoani Njombe na kuwa bado mazungumzo yanaendelea na wazalishaji wa zao hilo mkoani humo. Alibainisha kuwa mpango wao ni kuongeza uuzaji wa kahawa ya Tanzania katika migahawa hiyo kwa kuwa imeonekana kupendwa na wateja wao walio wengi.
Kwa upande wake, Balozi Luvanda aliwashukuru OBSCURA kwa ushirikiano mzuri wa kuimarisha biashara ya kahawa ya Tanzania nchini Japan na kwa jitihada zao za kuitangaza kahawa hiyo kwa walaji wa Japan. Aliwahakikishia ushirikiano wa Ubalozi watakaohitaji kwa wakati wote kwa kuwa jukumu kubwa la ubalozi ni kuendelea kutafuta masoko ya bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini ikiwemo, mazao ya kilimo kama kahawa.