Tarehe 18 Machi 2023, Ubalozi ulishiriki kwenye Tamasha la Hisani lililoandaliwa na Wenza wa Mabalozi wa Nchi za Afrika zenye Uwakilishi nchini Japan (Association of Wives of African Ambassadors in Japan - AWAAJ) lijulikanalo, “African Charity Bazaar”. Matamasha ya aina hii huandaliwa kila mwaka kwa lengo la kusaidia makundi yenye mahitaji maalum barani Afrika na nchini Japan, kupitia viingilio vya tamasha hilo.
Kwa mwaka huu, tamasha hilo liliratibiwa na kufanyika Ubalozi wa Angola ambapo Balozi 15 za Kiafrika na Asasi zipatazo 10 zisizo za Kiserikali za nchini Japan zilishiriki.
Ubalozi ulitumia tamasha hilo kutangaza vivutio vya utalii kupitia filamu ya Tanzania – The Royal Tour pamoja na bidhaa zinazozalishwa nchini ikiwemo, kahawa, chai, korosho na vyakula vya kitanzania.
Ubalozi umekuwa ukishirikiana na Umoja wa Jumuiya za Kibalozi zilizopo Japan kama vile Jumuiya ya Balozi za Kiafrika (African Diplomatic Corps – ADC); Umoja wa Balozi wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC); na Balozi za Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Majukwaa na matamasha ya Jumuiya hizo yamekuwa yakitumika kutangaza vivutio vya utalii, bidhaa zinazozalishwa katika nchi za Afrika pamoja na kuwakutanisha wawekezaji wa kijapani kwa pamoja, kwa lengo la kuwavutia kuwekeza katika nchi wanachama.