Tarehe 15 Oktoba 2023, Timu ya Riadha ya Tanzania imeshiriki katika Mashindano ya Nagai Marathon 2023, yaliyofanyika katika Jiji la Nagai, Yamagata, Japan. Timu hiyo imewajumuisha wanariadha sita wakiwemo, Peter Sulle, Fabian Joseph, Sara Ramadhan, Josephat Gisemo, Paul Makiya na Transfora Ngimbudzi na viongozi wawili, Kanali Mstaafu na Mwanahiri Mashuhuri Juma Ikangaa na Kocha wa timu hiyo Bw. Samson Nyonyi.

Aidha, Balozi wa Tanzania nchini Japan, Mheshimiwa Baraka Luvanda aliambatana na Afisa Ubalozi, Bi. Edna Dioniz Chuku na kujumuika na timu ya Tanzania jijini Nagai.

Mashindano hayo ya “Nagai Marathon 2023” yaliyoandaliwa na Halmashauri ya Jiji la Nagai, yalishirikisha wanariadha wapatao 600 kutoka Japan na Tanzania kwa lengo la kukuza ushirikiano katika sekta ya michezo. 
Wanariadha Peter Sulle na Fabian Joseph waliibuka kidedea kwa ushindi wa nafasi ya kwanza na ya pili kwa mbio za Kilometa 42, mtawalia. Aidha, wanariadha Josephat Gisemo na Paul Makiya waliibuka kidedea kwa ushindi wa kwanza na wa pili kwa mbio za Kilometa 21, mtawalia. Kwa upande wa Marathoni ya Wanawake ya Kilometa 42, mwanariadha Sara Ramadhan aliibuka mshindi wa kwanza, na huku  mwanariadha Transfora Ngimbudzi akiibuka mshindi wa kwanza kwa mbio za Kilometa 21 na kujiwekea rekodi yake tangu kuanza kukimbia mbio za urefu huo.

Wakifungua mashindano hayo, Mheshimiwa Baraka Luvanda, Balozi wa Tanzania nchini Japan na Mstahiki Meya wa Jiji la Nagai, Shigeharu  Uchiya walielezea umuhimu wa michezo katika kukuza diplomasia kimataifa na namna ambavyo, inavyoweza kuunganisha tamaduni, kujenga uhusiano na kudumisha ushirikiano kimataifa. 

Balozi Luvanda aliyaelezea mashindano hayo kuwa yana umuhimu mkubwa katika kukuza vipaji kwa wanamichezo wa Tanzania pamoja na kudumisha uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Japan. Alitoa hamasa kwa wanariadha hao na kueleza kuwa kupitia ushiriki wao katika michezo wao ni Mabalozi wa Taifa letu kwa kuwa wamebeba dhamana ya kuitambulisha na kuitangaza Tanzania, duniani. Aidha, alielezea hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kukuza sekta ya michezo nchini, ikiwemo, ujenzi na ukarabati wa miundombinu mbalimbali ya michezo, na ushirikishwaji wa vijana na wanawake katika maendeleo ya sekta hiyo.

Tanzania na Jiji la Nagai zimekuwa na ushirikiano uliodumu kwa muda mrefu tangu mwaka 2015 ukiwa na manufaa kwa pande zote mbili kupitia nyanja za kijamii, sanaa, michezo na utamaduni. Mathalan, mwaka 2019 Jiji la Nagai uliialika timu ya riadha ya Tanzania kushiriki kwenye mashindano ya “Nagai Marathon 2019”; na pia mji huo ulikuwa mwenyeji wa Timu ya Taifa ya Olimpiki ya Tanzania iliyoshiriki katika Michezo ya Olimpiki ya Tokyo 2020. 

Hata baada ya kuhitimishwa kwa Mashindano ya Olimpiki ya Tokyo 2020, Mji wa Nagai umeendeleza mawasiliano ya karibu na Tanzania na kurasimisha ushirikiano kati ya mji huo wa Nagai na Baraza la Michezo Tanzania; na hivyo kuwezesha fursa za mafunzo ya michezo kwa wataalamu wa Tanzania mjini Nagai. Aidha, mji wa Nagai umedhamiria kuwa na ushirikiano wa kidada (sistership) kati yake na jiji la Dodoma na hivyo kufungua fursa nyingi za ushirikiano zitakazonufaisha pande husika.

Mashindano haya ya Nagai Marathon ni sehemu ya maandalizi ya Mashindano ya Olimpiki yatakayofanyika mwakani, Paris, Ufaransa.