Tarehe 19 Novemba 2024, Ubalozi kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Chemba ya Biashara ya Afrika na New Zealand (ANZBC) uliandaa Kongamano la Uwekezaji lililofanikisha kuunganisha wadau mbalimbali wa uwekezaji na biashara kutoka New Zealand na Tanzania.
Mhe. Balozi Baraka Luvanda, Balozi wa Tanzania anayeiwakilisha New Zealand kutokea Tokyo, Japan pamoja na Mhe. Philip Hewitt, Balozi wa New Zealand anayeiwakilisha Tanzania, kutokea jijini Pretoria, South Afrika; waliombatana na Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania nchini New Zealand, Bw. Stuart Batty na Mwakilishi wa Heshima wa New Zealand nchini Tanzania, Bw. Kalpesh Mehta, walishiriki Kongamano hilo.
Wawekezaji wapatao 50 kutoka New Zealand walioshiriki Kongamano hilo, lililofanyika kwa njia ya mtandao, walipata fursa ya kubaini na kuchangamkia fursa za kibiashara na uwekezaji zinazopatikana nchini Tanzania.
Tanzania ina wawekezaji kutoka New Zealand waliowekeza katika sekta za TEHAMA (ICT), sayansi na teknolojia, utalii, kilimo, ufugaji, nishati, madini, huduma, viwanda na usafirishaji. Kufanyika kwa Kongamano hili ni mwendelezo wa jitihada za kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi baina ya nchi hizi mbili.