Tanzania imeshiriki Maonesho ya Kimataifa ya Kahawa Japan yanayojulikana 2022 Japan Specialty Coffee Conference & Exhibition yaliyoanza tarehe 12 Oktoba 2022 na kuhitimishwa tarehe 14 Oktoba 2022 jijini Tokyo, Japan. Maonesho haya ya kimataifa ya kahawa Japan yameandaliwa na Taasisi ya Kahawa ya Japan (Specialty Coffee Association of Japan – SCAJ) na kushirikisha makampuni na taasisi zinazohusika na kahawa zipatazo 235 kutoka nchi zinazozalisha kahawa duniani. 

Bodi ya Kahawa Tanzania (Tanzania Coffee Board) imeshiriki pamoja na wawakilishi wa vyama viwili vya ushirika na makampuni matatu ya Kitanzania yanayohusika na uzalishaji na uuzaji wa kahawa yakiwemo, Kagera Cooperative Union (KCU), Karagwe District Cooperative Union (KDCU), Kampuni ya Kaderes Peasants Development (KPD), Kampuni ya Acacia na Kampuni ya Touton Tanzania Ltd. 

Katika maonesho haya, Tanzania ilikua na banda maalum la kuonesha bidhaa za kahawa zinazozalishwa Tanzania ambazo zinajumuisha kahawa iliyochakatwa katika hatua za awali (green coffee) kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania. Vilevile, kupitia maonesho hayo ilioneshwa na kutangazwa kahawa iliyotayari kwa ajili ya matumizi ikiwemo, kahawa mumunyifu (instant coffee) inayozalishwa na viwanda vikubwa vya kukaanga kahawa nchini Tanzania vya Amimza na Tanica. 

Katika siku ya pili ya maonesho hayo, tarehe 13 Oktoba 2022, Tanzania ilipata fursa ya kufanya warsha maalum kuhusu kahawa ya Tanzania iliyoambatana na zoezi la uonjaji wa sampuli za kahawa za Tanzania (Tanzania Coffee seminar and cupping session) kwa makampuni yapatayo 60 ya ukaangaji (coffee roasters) na usafirishaji kahawa ya nchini Japan. Katika tukio hilo, sampuli za kahawa za wazalishaji na makampuni ya Tanzania yapatayo 26 zimeoneshwa, kutangazwa na kuonjwa kwenye siku hiyo iliyotengwa maalum kwa ajili ya kuitangaza kahawa ya Tanzania. Sampuli hizo ni za kahawa ya Arabica laini (full washed), Arabica ngumu (naturals) na kahawa ya Robusta. 

Makampuni ya Japan yameonesha kuvutiwa na kahawa ya Tanzania na kuanza hatua za awali za manunuzi ya kahawa hiyo yenye umaarufu nchini Japan. Hii ni fursa adhimu katika kukuza soko la kahawa ya Tanzania nchini Japan ambayo ni kahawa pendwa iliyopewa jina maarufu la kibiashara la “Tanzania Kilimanjaro Coffee”. 

Kutokana na mapokeo makubwa ya kahawa ya Tanzania katika maonesho haya, soko la kahawa ya Tanzania nchini Japan linatarajiwa kuongezeka kutoka asilimia 32 inayouzwa sasa Japan ambayo ni sawa na wastani wa kilogramu 15,000,000 inayouzwa kwa mwaka. Kiwango hiki kimeelezwa kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi tatu zinazouza kwa wingi kahawa yake nchini Japan.