Leo, tarehe 09 Oktoba 2024, Mheshimiwa Baraka Luvanda, Balozi wa Tanzania nchini Japan ameungana na mabalozi pamoja na viongozi mbalimbali wa nchi zinazozalisha kahawa duniani, kwenye hafla ya ufunguzi wa Maonesho ya 21 ya Kimataifa ya Kahawa nchini Japan (2024 Japan Specialty Coffee Conference & Exhibition) iliyofanyika jijini Tokyo, Japan.  Katika ufunguzi huo Mhe. Balozi Baraka Luvanda aliambatana na Bw. Primus Kimaryo, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB). 

Maonesho ya Kimataifa ya Kahawa Japan yameandaliwa na Taasisi ya Kahawa ya Japan (Specialty Coffee Association of Japan – SCAJ) na kushirikisha makampuni na taasisi zinazohusika na kahawa zipatazo 250 kutoka nchi zinazozalisha kahawa duniani. Maonesho haya yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 11 Oktoba 2024; na kuhudhuriwa na wadau wa kahawa wapatao 45,000 wakiwemo, wazalishaji, wanunuzi na wasafirishaji wa zao hilo.

Tanzania inawakilishwa na Bodi ya Kahawa Tanzania (Tanzania Coffee Board) ambayo, imeshiriki pamoja na wawakilishi wa vyama vya ushirika na makampuni ya Kitanzania yanayohusika na uzalishaji, usafirishaji, uuzaji na ufungashaji wa kahawa yakiwemo, Kilimanjaro Cooperative Union, Kampuni ya Kaderes Peasants Development (KPD), na Kampuni ya TANJA.

Aidha, katika maonesho hayo, Tanzania ina banda maalum la kuonesha bidhaa za kahawa zinazozalishwa Tanzania, zinajumuisha kahawa iliyochakatwa katika hatua za awali (green coffee) kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania. Pia, kupitia maonesho hayo inaoneshwa na kutangazwa kahawa iliyo tayari kwa ajili ya matumizi ikiwemo, kahawa mumunyifu (instant coffee) inayozalishwa na viwanda vikubwa vya kukaanga kahawa nchini Tanzania vya Amimza, Afri Café na Tanica. 

Vilevile, siku ya pili ya maonesho hayo tarehe 10 Oktoba 2024,  Tanzania itapata fursa ya kufanya semina maalum kuhusu kahawa ya Tanzania itakayoambatana na zoezi la uonjaji wa sampuli za kahawa za Tanzania (Tanzania Coffee Seminar and Cupping Session) kwa makampuni yapatayo 80 ya ukaangaji (coffee roasters) na usafirishaji kahawa ya nchini Japan. Katika tukio hilo, sampuli za kahawa za wazalishaji na makampuni ya Tanzania yapatayo 35 zitaoneshwa, kutangazwa na kuonjwa kwenye siku hiyo iliyotengwa maalum kwa ajili ya kuitangaza kahawa ya Tanzania. Sampuli hizo ni za kahawa ya Arabica laini (full washed), Arabica ngumu (naturals) na kahawa ya Robusta.