Leo, tarehe 14 Novemba 2023, Mheshimiwa Balozi Baraka Luvanda ameshiriki kwenye Mkutano wa Tatu (03)  wa Maandalizi (3rd International Planning Meeting – IPM) ya Maonesho ya Biashara ya Dunia ya Mwaka 2025 (EXPO 2025 OSAKA, KANSAI), jijini Osaka, Japan. Balozi Luvanda alishiriki mkutano huo akiambatana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Bi. Latifa Mohammed ambaye pia ni Kamishna Mkuu wa Maandalizi ya Tanzania katika Maonesho hayo; Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania katika jiji la Osaka, Dr. Kazusue Konoike; na Maafisa Waandamizi kutoka TANTRADE na Ubalozi wa Tanzania nchini Japan.

Washiriki wa Mikutano hii ni Taasisi za Ukuzaji Biashara (Trade Promotions – TPOs) duniani ambazo zinatoka kwenye Nchi Wanachama wa Shirikisho la Maonesho ya Biashara Duniani (Bureau for International Exhbitions – BIE). Jumla ya TPOs 501 zimeshiriki mkutano huu unaoendelea kwa muda wa siku 3.

Katika Mkutano huu, nchi ishirini na tano (25) zimetia saini mikataba ya ushiriki wa Maonesho ya EXPO 2025 OSAKA, KANSAI ikiwemo, Tanzania. Bi. Latifa Khamis Mohamed, Mkurugenzi Mkuu - TANTRADE ametia saini mkataba huo kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Inatarajiwa kuwa Tanzania itashiriki Maonesho hayo ya EXPO 2025 OSAKA, KANSAI yaliyopangwa kufanyika jijini Osaka, Japan, kuanzia tarehe 13 Aprili hadi 13 Oktoba 2025, kwa mada inayohusu “Connecting Lives” (chaguo la kwanza)  na “Empowering Lives” (chaguo la pili) pamoja na Siku ya Kitaifa inayopendekezwa kwa tarehe za mwezi Mei 2025. 

Tanzania inatarajiwa kutumia fursa za Maonesho haya makubwa ya EXPO 2025 OSAKA, KANSAI kujitangaza kwa kuonesha bidhaa za kimkakati, kuunganisha uzalishaji na masoko na kutangaza vivutio na fursa za uwekezaji ili kukuza biashara na uchumi wa Taifa.

Kwa upande wa Ubalozi, unaendelea kuratibu kwa ukaribu maandalizi na ushiriki wa Tanzania katika Maonesho hayo kwa kushirikiana na TANTRADE na taasisi zingine zinazohusika nchini. Mkutano huu wa Maandalizi ni wa tatu (03) kufanyika jijini Osaka (3rd IPM) utakaohitimishwa tarehe 16 Novemba 2023, umetanguliwa na mkutano wa pili (2nd IPM) uliofanyika mwezi Juni 2023, na mkutano wa kwanza (1st IPM) uliofanyika mwezi Oktoba 2022.