Tarehe 25 - 27 Juni 2024, Tanzania ilishiriki kwenye Mkutano wa Maandalizi (International Participants Meeting - IPM) ya Maonesho ya Dunia 2025, yajulikanayo “EXPO 2025 Osaka, Kansai, Japan”, uliofanyika jijini Nara, Japan. Mkutano huo umehudhuriwa na washiriki wapatao 600 kutoka nchi takriban 160 duniani, ukiwa na lengo la kutoa taarifa kuhusu uandaaji wa mabanda ya Maonesho kwa washiriki; na kujadili hatua za maandalizi ya Maonesho husika kutoka kwa waandaaji pamoja na nchi washiriki.
Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo uliongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil T. Abdallah aliyeambatana na Balozi wa Tanzania nchini Japan, Mhe. Baraka H. Luvanda pamoja na maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Ubalozi wa Tanzania nchini Japan na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE).
Maonesho hayo ya Dunia 2025 (EXPO 2025) yanatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 13 Aprili hadi 13 Oktoba, 2025 Osaka, Kansai, Japan katika kisiwa cha Yumeshima. Maonesho haya yanalenga kutangaza fursa mbalimbali zipatikanazo duniani ambayo, yamebeba kauli mbiu ya “Kubuni jamii ya Baadaye kwa Maisha Yetu (Designing Future Society for Our Lives)”; inayowiana na malengo ya SDGs ya Umoja wa Mataifa ambayo, lengo kuu ni kupata maendeleo jumuishi na endelevu na kuhakikisha hakuna atakayeachwa nyuma.
#IPM2024 #IPM
#EXPO2025isComing #くるぞ万博 #EXPO2025 #大阪関西万博 #ミャクミャク #myakumyaku
#JAPAN #TANZANIA