Leo, tarehe 10 Oktoba 2024, jijini Tokyo, pembezoni mwa Maonesho ya Kimataifa ya Kahawa Japan (SCAJ) 2024, ikiwa ni siku ya pili ya Maonesho hayo, kumefanyika Semina Maalum kuhusu Kahawa ya Tanzania iliyoambatana na zoezi la uonjaji kahawa inayozalishwa nchini (cupping).
Semina hiyo imeendeshwa na Balozi Baraka Luvanda na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Bw. Primus Kimaryo; na kuhudhuriwa na wadau wa kahawa wa nchini Japan wapatao 50.
Imebainishwa kuwa kahawa ya Tanzania inaendelea kujipatia umaarufu mkubwa nchini Japan na kuwa ni mnunuzi mkubwa na namba moja wa kahawa yote inayolimwa nchini kwa zaidi ya asilimia 34.
Semina hiyo ni sehemu ya Kampeni ya Kuitangaza Kahawa ya Tanzania nchini Japan inayoendeshwa kwa ushirikiano baina ya Ubalozi na Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB).