Leo, tarehe 28 Septemba 2023, ikiwa ni siku ya pili ya Maonesho ya Kimataifa ya Kahawa nchini Japan (2023 Japan Specialty Coffee Conference & Exhibition), yaliyofunguliwa jana tarehe 27 Septemba 2023 jijini Tokyo, Japan, imeweza kufanyika semina maalum na zoezi la uonjaji wa sampuli za kahawa ya Tanzania kutoka kwa kampuni wazalishaji zipatazo 30 nchini. Sampuli hizo ni kahawa ya Arabica laini (full washed), Arabica ngumu (naturals) na kahawa ya Robusta.
Siku hii iliyokuwa maalum kwa ajili ya kuitangaza kahawa ya Tanzania kwa wadau wa kahawa nchini Japan na washiriki wengine wa Maonesho hayo kupitia semina maalum iliyoandaliwa kwa ajili ya Tanzania, imeweza kupata mwitikio mkubwa kwa kuhudhuriwa na wadau wa kahawa wapatao 80 wa ndani na nje ya Japan.
Mheshimiwa Baraka Luvanda, Balozi wa Tanzania nchini Japan amefungua semina hiyo kwa kuinadi Tanzania pamoja na vivutio vyake ambapo nchini Japan, kahawa ya Tanzania ni miongoni mwa vivutio hivyo; iliyoweza kujipatia umaarufu mkubwa kwa radha na ubora wake na kupewa Jina la Kibiashara la Tanzania Kilimanjaro Coffee. Jina hili hutumika nchini Japan, kwa kahawa zinazozalishwa Tanzania pekee, kwa kutambua kivutio kikubwa cha Mlima Kilimanjaro uliopo nchini Tanzania. Balozi Luvanda pia ameweza kutumia fursa hiyo, kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji wa Japan, kufanya biashara na kuwekeza nchini kwenye zao hilo na mazao mengine ya kimkakati.
Tanzania inasifika Japan kwa kutoa kahawa bora aina ya Arabica (Arabica laini - full washed na Arabica ngumu - natural) inayolimwa katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Mara, Tanga, Morogoro, Njombe, Iringa, Katavi, Rukwa, Ruvuma, Kigoma, Songwe na Mbeya; na kahawa ya Robusta inayolimwa mkoani Kagera.
Tanzania imeweza kushiriki katika Maonesho hayo ya Kimataifa ya Kahawa kama mdau mkubwa wa kahawa duniani ambapo, kwa mwaka huu yametimiza miaka 20 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2003. Mwaka huu, yameshirikisha makampuni na taasisi zinazohusika na kahawa zipatazo 250 kutoka nchi zinazozalisha kahawa duniani na kuhudhuriwa na wadau wa kahawa wapatao 45,000 wakiwemo, wazalishaji, wanunuzi na wasafirishaji wa zao hilo. Aidha, yanatarajiwa kuhitimishwa kesho, tarehe 29 Septemba 2023.
Tanzania inawakilishwa na Bodi ya Kahawa Tanzania (Tanzania Coffee Board) ambayo, imeshiriki pamoja na wawakilishi wa vyama vya ushirika na makampuni ya Kitanzania yanayohusika na uzalishaji, usafirishaji, uuzaji na ufungashaji wa kahawa yakiwemo, Kagera Cooperative Union (KCU), Kampuni ya Kaderes Peasants Development (KPD), Kampuni ya Kamal Agro, Kampuni ya TANJA, Kampuni ya Ubumwe na Kampuni ya Interbulk Packaging.
Vilevile, katika maonesho hayo, Tanzania ina banda maalum la kuonesha bidhaa za kahawa zinazozalishwa Tanzania, zinajumuisha kahawa iliyochakatwa katika hatua za awali (green coffee) kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania. Pia, kupitia maonesho hayo inaoneshwa na kutangazwa kahawa iliyo tayari kwa ajili ya matumizi ikiwemo, kahawa mumunyifu (instant coffee) inayozalishwa na viwanda vikubwa vya kukaanga kahawa nchini Tanzania vya Amimza, Afri Café na Tanica.
Kutokana na mapokeo makubwa ya kahawa ya Tanzania katika maonesho hayo, soko la kahawa ya Tanzania nchini Japan linatarajiwa kuongezeka kutoka asilimia 32 inayouzwa sasa Japan, ambayo ni sawa na wastani wa kilogramu 15,000,000 (tani 15,000) inayouzwa kwa mwaka nchini humo.