Leo, tarehe 29 Septemba 2023, ni siku ya tatu ya Maonesho ya Kimataifa ya Kahawa nchini Japan (2023 Japan Specialty Coffee Conference & Exhibition), yaliyofunguliwa tarehe 27 Septemba 2023 jijini Tokyo. Tanzania imeendelea kuonesha kahawa inayozalishwa nchini kupitia Maonesho hayo ambapo, imeonekana kuvutia wahudhuriaji wengi.
Kutokana na mapokeo makubwa ya kahawa ya Tanzania katika maonesho hayo, soko la kahawa ya Tanzania nchini Japan linatarajiwa kuongezeka kutoka asilimia 32 inayouzwa sasa Japan, ambayo ni sawa na wastani wa kilogramu 15,000,000 (tani 15,000) inayouzwa kwa mwaka nchini humo.
Maonesho hayo, ni fursa adhimu katika kukuza soko la kahawa ya Tanzania nchini Japan ambayo ni kahawa pendwa iliyopewa jina maarufu la kibiashara la “Tanzania Kilimanjaro Coffee”. Jina hili hutumika nchini Japan, kwa kahawa zinazozalishwa Tanzania pekee, kwa kutambua kivutio kikubwa cha Mlima Kilimanjaro uliopo nchini Tanzania.
Tanzania inasifika Japan kwa kutoa kahawa bora aina ya Arabica (Arabica laini - full washed na Arabica ngumu - natural) inayolimwa katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Mara, Tanga, Morogoro, Njombe, Iringa, Katavi, Rukwa, Ruvuma, Kigoma, Songwe na Mbeya; na kahawa ya Robusta inayolimwa mkoani Kagera.