Tarehe 29 Oktoba 2023, wakati wa kuhitimisha Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Japan (Japan Tourism EXPO 2023), yaliyofanyika tarehe 26 - 29 Oktoba 2023 jijini Osaka,  Mheshimiwa Balozi Baraka Luvanda alifanya mahojiano maalum na Shirika la Utangazaji la Japan - NHK, Idhaa ya Kiswahili kuelezea mwenendo wa utalii kwa wajapani nchini Tanzania.

Maongezi hayo yalijikita katika kuelezea jitihada za Serikali ya Tanzania katika kuendeleza sekta ya utalii nchini; fursa ya Maonesho ya Utalii ya Kimataifa ya Swahili (Swahili Internation Tourism Expo – S!TE) ya mwaka 2024 yatakayofanyika nchini mwezi Oktoba 2024; pamoja na jitihada za Ubalozi za kutafuta watalii kutoka Japan kwenda Tanzania.

Mahojiano hayo yalishirikisha pia wawakilishi kutoka taasisi za Tanzania zinazoshughulikia sekta ya utalii zilizoshiriki Maonesho hayo zikiwemo, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).