Ubalozi wa Tanzania nchini Japan ulihitimisha maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yaliyoanza tarehe 7 Julai 2022 kwa kuwakutanisha wadau wa Kiswahili wa nchini Japan, Diaspora na Wanadiplomasia mbalimbali kushuhudia matukio mbali mbali yaliyofanyika katika ofisi za ubalozi mjini Tokyo, tarehe 9 Julai 2022. Matukio hayo yalijumuisha hotuba mbalimbali; mahojiano maalumu ya Shirika la Utangazaji Japan (NHK); maonesho ya bidhaa, utalii, utamaduni na Filamu ya The Tanzania - Royal Tour; pamoja na vyakula na vinywaji vya Kitanzania vilivyoandaliwa kwa ajili ya kusheherekea siku hiyo.
Ubalozi uliandaa shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwashindanisha wazungumzaji wa Kiswahili wa nchini Japan kutoka makundi mbalimbali yakihusisha wanafunzi wanaosomea Kiswahili, Wajapan walioishi nchini Tanzania na wengine wanaojifunza Kiswahili sehemu mbalimbali za Japan. Jumla ya washiriki wa shindano la wazungumzaji Kiswahili walikuwa 11 ambao walichujwa kutoka idadi ya waliojitokeza wapatao 22 waliowasilisha mada mbalimbali kwa maandishi kwa kutumia lugha ya Kiswahili.
Pamoja na kuwatangaza na kuwapatia zawadi washindi watatu (3) wa shindano hilo, ubalozi ulitoa zawadi nyingine ndogo ndogo kwa washiriki wengine wote ikiwa ni katika kuwa hamasisha zaidi kushiriki katika mashindano hayo wakati mwingine. Mshindi wa kwanza wa Shindano hilo alikuwa Bi. Masami Sumi aliyewasilisha mada inayohusu “Utamaduni wa Kiswahili unaunganisha Watu”; nafasi ya pili ilichukuliwa na Bi. Megumi Yama, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha OSAKA, miongoni mwa vyuo vikuu vinavyofundisha Lugha ya Kiswahili nchini Japan, mada yake ilihusu "Kanga: Vazi linalovutia katika Utamaduni wa Kiswahili"; na nafasi ya tatu ilienda kwa Bi. Yasuko Togashi, ambaye aliwasilisha mada inayohusu “Nimechoka Kidogo - Watoto wa Kiswahili wana Upendo na Urafiki wakanisaidia”.
Maadhimisho haya ya Siku ya Kiswahili ni ya kwanza kufanyika, tangu Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) mnamo tarehe 23 Novemba 2021, kuipitisha kuwa na Siku yake maalum ya kuadhimishwa Kimataifa ambayo ni tarehe 7 Julai, kila mwaka.
Picha za washiriki wa Shindano la kuwasilisha mada kwa Lugha ya Kiswahili
Washindi wa Shindano la Kuwasilisha Mada kwa Lugha ya Kiswahili wakipewa zawadi na mkono wa pongezi
Balozi Luvanda akitoa zawadi kwa washiriki wengine wa Shindano ikiwa ni katika kuwa hamasisha zaidi kujifunza na kuwafundisha wengine Lugha ya Kiswahili