Tarehe 2 Julai 2023, Ubalozi ulizindua “Wiki ya Kiswahili Japan" ambayo, imehitimishwa leo tarehe 7 Julai 2023 ikiwa ni kilele cha Maadhimisho ya  Siku ya Kiswahili Duniani. Maadhimisho hayo, yaliyoanza tarehe 2 Julai 2023, yamewakutanisha wadau wa Kiswahili wa nchini Japan, Diaspora na Wanadiplomasia kushuhudia matukio mbalimbali ya kuenzi Lugha ya Kiswahili yaliyofanyika katika Ofisi za Ubalozi, jijini Tokyo.  

Washiriki hao ni Mabalozi na wawakilishi wa Balozi wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zenye uwakilishi Japan (Rwanda, Uganda, Sudani Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Kenya), Maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Japan wanaoshughulikia Dawati la Tanzania na masuala ya Kiswahili, wawakilishi wa Ofisi ya Meya wa Jiji la Nagai, Wajapani wakujitolea, walioishi au kufanya kazi nchini Tanzania, wanafunzi wa vyuo vikuu vya Japan vinavyofundisha Kiswahili, marafiki wengine wa Tanzania kutoka Japan, Diaspora na Shirika la Taifa la Utangazaji la Japan (NHK World) - Idhaa ya Kiswahili.  

Maadhimisho ya mwaka huu yalipambwa kwa Tamasha la Lugha ya Kiswahili Japan ambalo, lilijumuisha uwasilishaji wa hotuba kwa Lugha ya Kiswahili kutoka kwa wajapani walioishi Tanzania; makala kuhusu Kiswahili na utamaduni wake kutoka kwa wanafunzi wa Kijapani wanaosoma Kiswahili katika vyuo vikuu vya Japan; semina kuhusu vivutio vya utalii wa Tanzania; na maonesho ya sanaa, utamaduni na burudani. 

Aidha, hotuba na makala zilizotolewa ziligusa maisha ya wajapani hao walivyokuwa nchini Tanzania; na uelewa mpana wa Lugha ya Kiswahili na utamaduni wake kwa wanafunzi wa kijapani wanaosoma Kiswahili nchini Japan, kutoka Chuo Kikuu cha OSAKA, Chuo Kikuu cha Mafunzo ya Kigeni Tokyo (TUFS), Chuo Kikuu cha SOKA na Chuo Kikuu cha Sophia.

Itarejewa kuwa tarehe 7 Julai ya kila mwaka, watanzania na wazungumzaji wa Kiswahili kote duniani, wanaadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani iliyotangazwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) mnamo tarehe 23 Novemba 2021, kuwa 7 Julai ni Siku ya Kuadhimisha Lugha ya Kiswahili Duniani.  Uamuzi huo wa UNESCO ni kuenzi mchango mkubwa wa lugha hii kwa watanzania, waafrika na wazungumzaji wote wa Kiswahili duniani ambao, wanakadiriwa kufikia milioni 200.