Leo, tarehe 7 Julai 2025, Tanzania kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa lugha ya Kiswahili nchini Japan, iliadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani katika Maonesho ya Dunia ya EXPO 2025, yanayoendelea kisiwani Yumeshima, jijini Osaka, Japan. Maadhimisho haya yaliambatana pia na hafla rasmi ya kufunga Wiki ya Utamaduni na Kiswahili, iliyokuwa sehemu ya maonyesho hayo ya kimataifa chini ya Kaulimbiu: “Kiswahili kwa Amani na Mshikamano.”
Hafla hiyo ilihudhuriwa na wadau wa Kiswahili kutoka vyuo vikuu mbalimbali vya Japan, wanataaluma, wanafunzi, wanadiaspora wa Kitanzania, wanadiplomasia kutoka nchi mbalimbali za nchi za Jumuiyay a Afrika Mashariki (EAC), pamoja na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa kama vile UNESCO. Mgeni Rasmi wa tukio hilo alikuwa Mheshimiwa Baraka Luvanda, Balozi wa Tanzania nchini Japan.
Katika hotuba yake, Balozi Luvanda alisisitiza kuwa Kiswahili ni zaidi ya lugha; ni kiungo cha urithi wa utambulisho wa Taifa la Tanzania na Afrika kwa ujumla. Alieleza kuwa kukua kwa Kiswahili katika majukwaa ya kimataifa ni ushahidi wa nguvu ya lugha hiyo katika kujenga maelewano, mshikamano na amani baina ya mataifa. Aidha, aliipongeza UNESCO kwa kutambua rasmi tarehe 7 Julai kuwa Siku ya Kiswahili Duniani, pamoja na Serikali ya Japan kwa kuendeleza ushirikiano wa kiutamaduni na kitaaluma na Tanzania.
Katika kilele cha tukio hilo, Kamusi Ndogo ya Kiswahili-Kijapani ilizinduliwa rasmi kwa ushirikiano wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na Chuo Kikuu cha Osaka, kama mojawapo ya hatua za kuimarisha tafsiri na mawasiliano baina ya jamii mbili. Aidha, hati ya ushirikiano (MOU) kati ya SUZA na Chuo Kikuu cha Osaka ilisainiwa, ikishuhudiwa na Balozi Luvanda, ikiwa ni ishara ya kuimarika kwa ushirikiano wa kitaaluma baina ya Tanzania na Japan katika kukuza Lugha ya Kiswahili.
Maadhimisho hayo pia yalipambwa na burudani mbalimbali za kitamaduni zikiwemo mashairi ya Kiswahili, ngonjera kutoka kwa wanafunzi wa Kiswahili wa Chuo Kikuu cha Osaka, wimbo maalum kutoka Shule ya Awali ya SANAE, na ngoma kutoka kikundi cha JT-STARS. Hafla hii ilikuwa jukwaa la kuonesha ushawishi wa Kiswahili si tu kama lugha ya mawasiliano, bali pia kama nyenzo ya kuendeleza utamaduni, utalii, diplomasia na elimu ya kimataifa.
Katika kuwatambua wadau waliochangia kwa kiwango kikubwa katika kukuza Kiswahili nchini Japan, taasisi 11 na watu binafsi walitunukiwa Tuzo Maalum za BAKITA, zikitolewa na Mheshimiwa Balozi Luvanda. Waliopewa tuzo hizo ni pamoja na vyuo vikuu mashuhuri kama Osaka, Kyoto, TUFS, Waseda, Sophia, Soka, pamoja na Shirika la Utangazaji la Japan - NHK World (Idhaa ya Kiswahili), Bi. Midori Uno, na vikundi vya wanafunzi wa Kiswahili.
Maadhimisho haya yameonesha kwa vitendo dhamira ya Tanzania kuendelea kueneza Kiswahili duniani kupitia ushirikiano wa kimataifa, hususan kwa washirika wa maendeleo kama Japan. Ni matarajio ya wengi kuwa maadhimisho haya yataendelea kuleta msukumo mpya katika kukiweka Kiswahili katika safu za juu za lugha za kimataifa, sambamba na kuimarisha urafiki wa muda mrefu kati ya Tanzania na Japan.