Washiriki walipata nafasi ya kufuatilia Filamu ya The Tanzania - Royal Tour wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani
Majaji wa Shindano la Kuwasilisha Mada kwa Lugha ya Kiswahili
Maafisa Ubalozi wakionesha bidhaa za Tanzania kwenye Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani
Balozi Luvanda akiwa na Mabalozi na Wawakilishi wa Balozi wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wakiongozwa na Balozi Tabu Irina, Balozi wa Kenya - Japan na Mwenyekiti wa Mabalozi wa Nchi za EAC
Balozi Luvanda akimshukuru Bi. Midori Uno, Rafiki wa Tanzania, Mdhamini Mkuu na Jaji wa Shindano la Kuwasilisha Mada kwa Lugha ya Kiswahili
Balozi Luvanda akimshukuru Prof. Daisuke Shinagawa, Jaji wa Shindano na Mhadhiri wa Kiswahili wa Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Tokyo
Washiriki wakipata chakula na vinywaji vya Kitanzania vilivyoandaliwa kwa ajili ya kusheherekea siku hiyo
Washiriki wakitoa Heshima kama sehemu ya kumbukizi ya Hayati Shinzo Abe, Waziri Mkuu wa Zamani wa Japan

Tarehe 9 Julai 2022, Ubalozi wa Tanzania nchini Japan umehitimisha maadhimisho ya  Siku ya Kiswahili Duniani yaliyoanza tarehe 7 Julai 2022 kwa kuwakutanisha wadau wa Kiswahili wa nchini Japan, Diaspora na Wanadiplomasia mbalimbali kushuhudia matukio mbali mbali yaliyofanyika katika ofisi za  ubalozi mjini Tokyo.

Tarehe 7 Julai ya kila mwaka ilitangazwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) mnamo tarehe 23 Novemba 2021 kuwa ni Siku ya Kiswahili Duniani na katika kuadhimisha siku hiyo,Ubalozi uliandaa shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwashindanisha wazungumzaji wa Kiswahili wa nchini Japan kutoka makundi mbalimbali yakihusisha wanafunzi wanaosomea Kiswahili, Wajapan walioishi nchini Tanzania na wengine wanaojifunza Kiswahili sehemu mbalimbali za Japan. Jumla ya washiriki wa shindano la wazungumzaji Kiswahili walikuwa 11 ambao walichujwa kutoka idadi ya waliojitokeza wapatao 22 waliowasilisha mada mbalimbali kwa maandishi kwa kutumia lugha ya Kiswahili. 

Pamoja na kuwatangaza na kuwapatia zawadi washindi watatu (3) wa shindano hilo, ubalozi ulitoa zawadi nyingine ndogo ndogo kwa washiriki wengine wote ikiwa ni katika kuwa hamasisha zaidi kushiriki katika mashindano hayo wakati mwingine. Matukio mengine yaliyoambatana na hafla ya kuhitimishwa Siku ya Kiswahili yalikuwa ni pamoja na hotuba mbalimbali; mahojiano maalumu ya Shirika la Utangazaji Japan (NHK); maonesho ya bidhaa, utalii, utamaduni na Filamu ya The Tanzania - Royal Tour; pamoja na vyakula na vinywaji vya Kitanzania vilivyoandaliwa kwa ajili ya kusheherekea siku hiyo. 

Katika hotuba yake ya ukaribisho kwa wageni,Balozi Baraka Luvanda alitumia fursa hiyo kuwashukuru wageni wote, wadau na marafiki kwa kushiriki na kufanikisha maadhimisho hayo yaliyofanyika kwa mara ya kwanza tangu ilipotangazwa na UNESCO kuwa tarehe 7 Julai ya kila mwaka ni Siku ya Kiswahili Duniani. Balozi Luvanda aliwapongeza washiriki wa shindano kwa kuwasilisha mada nzuri na kwa kutumia kiswahili fasaha ikiwa ni kielelezo cha mapenzi na hamasa kubwa waliyonayo kwa lugha hiyo na akawaomba kuendeleza utamaduni huo na kuitangaza lugha hiyo pamoja na utamaduni wake. 

Aidha, Balozi Luvanda alitumia nafasi hiyo kuelezea historia fupi ya Lugha ya Kiswahili tangu kuanza kutumika kwake na kuenea katika vipindi mbalimbali hadi kutambuliwa na Umoja wa Mataifa kupitia UNESCO kuwa miongoni mwa lugha 10 yenye wazungumzaji wengi duniani wapatao milioni 200. Alieleza zaidi kuwa kiswahili sasa ni mojawapo ya lugha rasmi nane zinazotambulika na Umoja wa Mataifa kwa kupewa hadhi ya kuwa na Siku Maalum ya kuadhimishwa kimataifa na akabainisha kuwa lugha nyingine saba zenye hadhi hiyo ni: Kiingereza (23 Aprili); Kifaransa (20 Machi); Kichina (20 Aprili); Kiarabu (18 Disemba); Kireno (05 Mei);Kirusi (06 Juni) na Kispaniola (23 Aprili).

Katika mahojiano na Shirika la Utangazaji la Japan (sehemu ya lugha za kigeni), Balozi Luvanda alishukuru na kupongeza jitihada za Serikali ya Tanzania kwa kuieneza na kuitangaza lugha ya kiswahili duniani kote na akaeleza kuwa sasa Serikali inaandaa Mpango Mkakati wa Kuibidhaisha Lugha ya Kiswahili ndani na nje ya nchi. Akaeleza kuwa ni kwa muktadha huo, ubalozi umejipanga kutekeleza maelekezo ya Serikali ya kuanzisha vituo vya kufundishia kiswahili katika balozi zake zilizopo nje ya nchi. 

Balozi Luvanda alihitimisha kwa kuwaomba wadau na marafiki mbali mbali walioshiriki katika maadhimisho ya Siku ya Kiswahili kushiriki pamoja katika kufanikisha azma ya kuanzisha kituo hicho mjini Tokyo. 

Kabla ya kuanza kwa matukio ya maadhimisho hayo, washiriki waliombwa kusimama kimya kwa muda ikiwa ni sehemu ya kumbukizi ya Hayati Shinzo Abe, Waziri Mkuu wa Zamani wa Japan ambaye alifariki Dunia tarehe 8 Julai 2022 kufuatia shambulio la bunduki kutoka mmoja wa Japan huko katika Jimbo la Nara.

  • Picha ya baadhi ya washiriki wa Shindano la kuwasilisha mada kwa Lugha ya KiswahiliPicha ya baadhi ya washiriki wa Shindano la kuwasilisha mada kwa Lugha ya Kiswahili
  • Washindi wa Shindano la Kuwasilisha Mada kwa Lugha ya Kiswahili wakipewa zawadi na mkono wa pongeziWashindi wa Shindano la Kuwasilisha Mada kwa Lugha ya Kiswahili wakipewa zawadi na mkono wa pongezi
  • Balozi Luvanda akiwa na Bi. Midori Uno, Bw. Yoshiharu Matsumoto na Bi. Kuniko Shimizu, wadhamini wa Shindano la Kuwasilisha Mada kwa Lugha ya KiswahiliBalozi Luvanda akiwa na Bi. Midori Uno, Bw. Yoshiharu Matsumoto na Bi. Kuniko Shimizu, wadhamini wa Shindano la Kuwasilisha Mada kwa Lugha ya Kiswahili
  • Mhe. Balozi Luvanda katika picha  na Viongozi wa Diaspora pamoja na washiriki wa Shindano la Kiswahili katika Maadhimisho ya  Siku ya Kiswahili DunianiMhe. Balozi Luvanda katika picha na Viongozi wa Diaspora pamoja na washiriki wa Shindano la Kiswahili katika Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani
  • Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yalipambwa pia kwa maonesho ya Filamu ya The Tanzania - Royal Tour; vyakula na bidhaa za Kitanzania.Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yalipambwa pia kwa maonesho ya Filamu ya The Tanzania - Royal Tour; vyakula na bidhaa za Kitanzania.