HOTUBA YA UKARIBISHO KUTOKA KWA BALOZI BARAKA H. LUVANDA, BALOZI WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NCHINI JAPAN WAKATI WA MAADHIMISHO YA PILI (2) YA SIKU YA KISWAHILI DUNIANI,
UBALOZI WA TANZANIA, TOKYO, 2 JULAI 2023

Mheshimiwa Balozi Ernest RWAMUCYO,
Balozi wa Jamhuri ya Rwanda nchini Japan na Mwenyekiti wa Mabalozi wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki;

Mheshimiwa Tophace KAAHWA,
Balozi wa Jamhuri ya Uganda nchini Japan;

Mheshimiwa Akuei Pac Garang KURENG,
Balozi wa Jamhuri ya Sudan Kusini nchini Japan,

Ndugu Espé-Martin KAPONGO KAPONGO,
Kaimu Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) nchini Japan;

Bw. Zouga Seiling,
Mwakilishi wa Balozi wa Jamhuri ya Kenya nchini Japan;

Bw. Kenta Takashi
Afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Japan anayeshughulikia Dawati la Tanzania;

Bi. Fumiyo Jin
Afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Japan anayeshughulikia Masuala ya Kiswahili;

Bi. Midori Uno, 
Rafiki wa Tanzania,

Marafiki Wengine Wote wa Tanzania Mliopo hapa leo;

Wanafunzi kutoka Vyuo Vikuu vya Japan mliojumuika nasi  hapa leo;

Ndugu Zangu Wanadiaspora wa Tanzania nchini Japan;

Wageni  Waalikwa;

Mabibi na Mabwana.

Habari za Asubuhi! 
Jambo!
Konnichi wa!


Naomba nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa wingi wa rehema na baraka zake na kwa kutukutanisha kwa mara nyingine tena hapa leo hii.

Ninayo furaha tele kuwakaribisha nyote hapa ubalozini , mjisikie mpo nyumbani .

Aidha, ninapenda kuwashukuru nyote kwa dhati kabisa kwa kuamua kutumia muda wenu adhimu wa mapumziko ya mwisho wa wiki kuja kujumuika nasi katika hafla hii ya Siku ya Kiswahili Duniani.

Hii ni mara ya pili tunaadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani tangu ilipotamkwa na   Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) mwezi Novemba 2021 kuwa  tarehe 7 Julai ya kila mwaka itakuwa Siku ya Maadhimisho ya Kiswahili Duniani, ikiwa ni katika kutambua na kuenzi mchango mkubwa wa lugha hiyo katika kuwezesha mawasiliano ya watu wengi wanaoizungumza lugha hii.

Tarehe 9 Julai 2022 tuliadhimisha kwa mara ya kwanza siku hiyo ya Kiswahili kwa shughuli mbali mbali ikiwa ni pamoja na Shindano la Hotuba kwa lugha ya Kiswahili lililowaibua washiriki wapatao ishirini na mbili (22).

Ninafurahi kuona baadhi yenu mlishiriki pamoja nasi mwaka jana na leo hii hamkusita kujumuika tena nasi.

Kipekee, ninawashukuru sana Waheshimiwa Mabalozi kwa kuitikia mwaliko wetu na pia kwa kukubali kuzungumza machache wakati wenu utakapowadia. Tunasubiri kwa shauku kusikia salamu zenu kwa lugha yetu pendwa.

Ndugu Washiriki,

Mtaona kuwa tunaadhimisha Siku ya Kiswahili kwa namna tofauti na kwa tarehe tofauti. Tumefanya hivyo wala si kwa bahati mbayá, bali kwa makusudi.

Tumekusudia kufanya hivyo ili kuyafanya maadhimisho haya kuwa na hadhi ya kuwa Wiki ya Maadhimisho (Kiswahili Week) ambapo, leo tunaizindua rasmi na kuhitimishwa tarehe 7 Julai 2023.

Hivyo, tunatazamia pamoja na mambo mengine, tuwe na shughuli mbali mbali za kukienzi Kiswahili na utamaduni wa Kiswahili. Miongoni mwa shughuli hizo ni pamoja na kuwapa fursa rafiki zetu wa Japan wenye dhamira ya kujifunza lugha hii kutembelea Maktaba ndogo ya ya Ubalozi ili kuweza kujisomea vitabu mbalimbali vya lugha ya Kiswahili pamoja na kutoa elimu ya Kiswahili kupitia vyombo mbalimbali vya habari vya Japan ikiwemo, Shirika la Utangazaji la Japan - NHK, Idhaa ya Kiswahili ambao wamejumuika nasi leo hii.

Na kwa kweli NHK wamekuwa wadau wakubwa wa Ubalozi na tunawashukuru sana kwa kutupaisha kupitia vipindi vya Idhaa Kiswahili inayosikika sehemu mbali mbali duniani.

Kwa niaba ya wenzangu hapa ubalozini, ninapenda kuwashukuru wadau na marafiki wote ambao mmeshiriki pamoja nasi kwa michango yenu ya hali na mali iliyofanikisha maandalizi ya siku hii maalum na muhimu kwetu.Asanteni sana na niwatie shime  muendelee na moyo huo hata kwa siku zijazo.


Ndugu Wahiriki, Mabibi na Mabwana,

Naamini nitakuwa nimefanya kosa la kiitifaki endapo nitaacha kuwapongeza kwa dhati washiriki wote wa shughuli hii ya leo.

Kwanza, kwa namna mlivyoitikia mwaliko wetu kuja kuzungumza katika hadhara hii. Pili, kwa namna mlivyojipanga kwa hotuba, makala, tungo, tenzi, na maonesho ya sanaa na utamaduni wa kuenzi lugha hii adhimu. Ninawapongeza sana na ninaombea moyo wa ujasiri itakapowadia fursa ya kila mmoja wenu kuhutubia hadhara hii.

Mwaka huu tuliona kuwa kuwa ni vema tukaenzi mchango wenu mkubwa wa kuendeleza lugha ya Kiswahili hapa Japan pamoja na kupokea ushuhuda wa namna mlivyojifunza au kuelewa lugha na utamaduni wa Kiswahili. Mchango wenu katika kuendeleza Lugha ya Kiswahili ni ishara dhahiri ya mapenzi na hamasa kubwa mliyo nayo kwa lugha hii na utamaduni wake. Tunasubiri kwa hamasa kubwa kuwasikilizeni.

Na mwisho, japokuwa si kwa umuhimu, niwashukuru sana watumishi wenzangu ubalozini kwa maandalizi mazuri ya shughuli yetu hii na niwatie shime muendeleze kazi hii nzuri.

Ndugu Wageni Waalikwa; Mabibi na Mabwana,


Naomba mniruhusu, japokuwa kwa kifupi sana nirejee kuelezea historia na nafasi ya Kiswahili kama lugha ya Taifa la Tanzania na heshima tuliyopewa na UNESCO kwa kuichagua Siku Mahsusi ya Kuadhimisha Kiswahili Duniani.

Ninamini kuwa wengi wenu mnafahamu na huenda mtapenda kujua zaidi kuwa uamuzi wa kuichagua tarehe 7 Julai kuwa Siku ya Kiswahili duniani unatokana na historia yenyewe ya matumizi ya lugha ya Kiswahili nchini Tanzania.

Kimsingi,  uamuzi huu wa UNESCO unaweza kuelezwa kuwa unatokana na utashi wa kuienzi  tarehe 7 Julai 1954 ambayo ndiyo tarehe ya kuzaliwa kwa Chama cha TANU, chama kilichopigania uhuru wa Tanzania (wakati huo ikiitwa Tanganyika) chini ya uongozi wa Baba wa Taifa,  Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Hayati Mwalimu Nyerere anakumbukwa kwa kuchangia sana kuikuza na kuiendeleza lugha ya  Kiswahili nchini Tanzania na nje ya mipaka ya nchi kwa kuitumia katika harakati za kudai uhuru na ukombozi wa kiuchumi baada ya uhuru.

Aidha, baada ya kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika, Kiswahili kiliendelea kuwa kiunganisho muhimu kwa mataifa ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Jangwa la Sahara, kusini mwa Jangwa la Sahara katika harakati za kupigania uhuru katika mataifa hayo hata baada ya Tanganyika kupata uhuru wake mwaka 1961.

Ndugu Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana,

Hadi sasa, Kiswahili ni lugha rasmi ya Taifa na Serikali nchini Tanzania; na katika shule za msingi hutumika kama lugha ya kufundishia ambapo, kwa shule za sekondari pamoja na vyuo vikuu kinatumika kama lugha mojawapo ya mawasiliano.

Aidha, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inatambua lugha ya Kiswahili kama lugha ya mawasiliano mapana (lingua franca) kwa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo ambapo, shughuli nyingi za kijamii, biashara, jeshi, michezo na sanaa kufanyika kwa kutumia lugha hii.  Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Kiswahili kinatambulika kama lugha rasmi ya kazi ya Jumuiya ya SADC kuanzia mwaka 2018. Kukubalika kwa Kiswahili katika umoja huu, kunaifanya kuwa lugha ya nne katika Jumuiya hii. Vilevile, Umoja wa Afrika (AU) uliipitisha lugha ya Kiswahili, kuwa lugha rasmi ya kikazi ndani ya Umoja huo, mnamo tarehe 15 Februari 2022.

Ni dhahiri kuwa kukubalika huku kwa Lugha ya Kiswahili ndani ya Bara la Afrika kunasababisha Kiswahili kuwa na wazungumzaji wengi ambapo, hadi leo hii inao wazungumzaji takriban watu milioni 200 walio ndani na nje ya bara hili. Idadi hiyo inakifanya Kiswahili kuwa lugha ya tatu (03) kwa ukubwa Barani Afrika na moja ya lugha kumi (10) zinazozungumzwa zaidi duniani.

 


Ndugu Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,

Tanzania inachukua hatua madhubuti katika kukikuza Kiswahili na hata kuibidhaisha ndani ya nchi na duniani kote, kwa ujumla. Hivyo, napenda kutumia nafasi hii kupongeza jitihada za Serikali za Awamu mbalimbali za uongozi kwa kuwezesha Kiswahili kupiga hatua zaidi kitaifa na kimataifa.

Jitihada hizo ni pamoja na kuanzisha vyombo mbalimbali vya kusimamia na kuendeleza lugha hii; kutoa nyaraka mbalimbali za kitafiti na kitaaluma kuhusu Kiswahili; na kuimarisha mafunzo ya lugha kwa kutoa programu maalumu ya lugha ya Kiswahili zinazozalisha wataalam na watafsiri wa Lugha ya Kiswahili kwenye viwango vya kimataifa.

Ni faraja na fahari kubwa kuona Vilevile, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan imekuwa mstari wa mbele katika kuchagiza  jitihada za kuieneza lugha ya Kiswahili kitaifa na Kimataifa.

Kwa wale mnaofuatilia kwa karibu shughuli za kila siku za Umoja wa Afrika (AU) mtakuwa mnakumbuka katika Mkutano wa 36 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika mwaka huu (2023) mwezi Februari, jijini Addis Ababa, Ethiopia, Rais Samia alihutubia kwa Lugha ya Kiswahili.

Aidha,  Rais Samia alitumia fursa hiyo kuwashukuru Wakuu wa Nchi na Serikali kwa kupitisha Azimio la Kiswahili la Umoja wa Afrika ambapo, licha ya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya mawasiliano katika umoja huo.


Ndugu Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,


Katika kuunga mkono hatua hizo madhubuti za Serikali ya Tanzania za kukuza Kiswahili duniani, Ubalozi pia unafanya jitihada mbalimbali za kueneza lugha hiyo nchini Japan na maeneo mengine ya uwakilishi ikiwemo, kuandaa machapisho, mashindano ya insha kwa lugha ya Kiswahili, kushirikiana na vyombo vya habari katika kutoa vipindi vyenye mudhui ya Kiswahili; kushirikiana na Vyuo Vikuu pamoja na kuhamasisha Diaspora kufungua madarasa ya Kiswahili katika maeneo yetu ya uwakilishi.  

Napenda kujulisha hadhara hii kuwa ubalozi unaendelea kuhamasisha wanadiaspora kuchangia jitihada za kukikuza na kukiendeleza Kiswahili katika maeneo yote ya uwakilishi yaani Japan, Australia, New Zealand na Papua New Guinea.

Jitihada hizo ni pamoja na kuwapatia wadau wa Kiswahili nyenzo (vitabu, machapisho, vipeperushi n.k) kwa lengo la kurahisisha ufundishaji wa lugha fasaha. Aidha, tunakusudia kuwahamasisha wanadiaspora na marafiki wengine wa Tanzania katika kufikia azma ya kuanzisha Vituo vya Kufundisha Kiswahili kwenye nchi za uwakilishi.

Tunaamini vituo hivyo vitasaidia kuongeza idadi ya wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili zaidi kutoka idadi ya sasa inayotokana na wahitimu kutoka vyuo vikuu takribam sita (06) vya Japan pekee.

Na katika hili, naendelea kutoa wito kwenu - marafiki zetu, mliopo hapa leo na hata wale ambao hawakuweza kushiriki leo, kuendelea kushirikiana pamoja nasi ili hatimaye tuweze kuanzisha Kituo hicho hapa Japan.

Ndugu zangu Wageni Waalikwa,
 Mabibi na Mabwana,

Kama nilivyogusia hapo awali, mwaka huu, Ubalozi ulikusudia kuadhimisha kwa upekee wake siku hii muhimu ya Kiswahili kuanzia leo tarehe 2 Julai 2023 hadi kilele chake tarehe 7 Julai 2023, ili kuwapa nafasi ninyi mlio mabalozi  wa Lugha ya Kiswahili hapa Japan kuendelea kuwahamasisha Wajapani wengine waielewe na kuipenda lugha hii.

Kwa kutambua kuwa kilele cha Maadhimisho haya ni tarehe 7 Julai, ninaomba kutumia nafasi hii kutoa wito kwenu nyote kuendelea kuitumia na kuhamasisha matumizi ya lugha hii kwa umma wa Japan hata baada ya tarehe hiyo ili iendelee kueleweka na kufahamika kwa wajapani wengi.

Zaidi, ni matumaini yangu kuwa mtaendelea kuwa mabalozi wazuri wa lugha hii ndani na hata nje ya Japan. Naomba niwahakikisheni Ushirikiano wa Ubalozi wa Tanzania mtakaohitaji kwa muda wote.

Ndugu Wageni Waalikwa,Mabibi na Mabwana,


Naomba sasa kuhitimisha maneno haya machache kwa kuwashukuru, kwa mara nyingine, kwa kutupa fursa hii adhimu ya kujumuika pamoja na kuadhimisha Maadhimisho ya Pili (2) ya Siku ya Kiswahili Duniani.

 

Mungu Ibariki Afrika,
Mungu Ibariki Tanzania,
Mungu Ibariki Lugha yetu ya Kiswahili.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.