HOTUBA YA UKARIBISHO KUTOKA KWA
BALOZI BARAKA H. LUVANDA, BALOZI WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NCHINI JAPAN WAKATI WA HAFLA YA KUADHIMISHA SIKU YA KISWAHILI DUNIANI,
UBALOZI WA TANZANIA, TOKYO, 9 JULAI 2022
Mheshimiwa Balozi Tabu Irina,
Balozi wa Jamhuri ya Kenya nchini Japan na Mwenyekiti wa Mabalozi wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki;
Ndugu Espé-Martin KAPONGO KAPONGO,
Kaimu Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC);
Bw. Shadraque Wasike Mulijo,
Mwakilishi wa Balozi wa Jamhuri ya Uganda nchini Japan;
Bw. Soshi Katayama
Afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Japan anayeshughulikia masuala ya Tanzania;
Mama Midori Uno,
Rafiki wa Tanzania, Mdhamini na Jaji wa Shindano hili;
Profesa Daisuke Shinagawa,
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Tokyo na Jaji wa Shindano;
Mama Kuniko Shimizu,
Rafiki wa Tanzania na Mtendaji Mkuu wa Tanzaniaphilia;
Marafiki wengine wote wa Tanzania mliopo hapa;
Wanadiaspora wa Tanzania.
Ndugu Wageni Wote Waalikwa;
Mabibi na Mabwana.
Jambo!Konnichi wa!
I. HISANI
Ipo hadithi inayomhusu Profesa mmoja ambaye alikuwa na mazoea ya kuongea kwa kirefu. Siku moja aligundua kuwa mwanafunzi mmoja kwenye darasa lake alikuwa amesinzia. Akamuita mwanafunzi mmoja aliyekuwa ameketi jirani yake:
“John, unaweza kumuamsha huyo rafiki jirani na wewe?”
“Hapana, Prof.” Akajibu John. Muamshe wewe, Prof. Maana ni wewe uliyemfanya asinzie, sio mimi.”
Kwa hiyo ndugu Mshereheshaji kabla sijasababisha mtu yeyote kusinzia hapa nirhusu niongee maneno machache kama ifuatavyo:
Kwanza kabisa, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa wingi wa rehema na baraka zake ambazo zimetuwezesha kukutana hapa leo. Tunamrudishia Mungu sifa na utukufu wake.
Pili, naomba niwakaribishe nyote katika Ubalozi wa Tanzania hapa Tokyo, karibuni sana mjisikie mpo nyumbani.
Tatu, naomba nitoe shukrani zangu za dhati kwa kuchukua muda wenu wa mapumziko ya mwisho wa wiki kuja kujumuika nasi katika hafla hii fupi ya kuadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani. Hii ni mara ya kwanza kuadhimishwa tangu ilipotangazwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kuwa tarehe 7 Julai ya kila mwaka ni Siku ya Kiswahili Duniani.
Hata hivyo, mtaona kuwa tumeifanya leo tarehe 9 Julai siku tofauti na siku yenyewe lakini hiyo tumeifanya kwa minajili ya kuwezesha ushiriki wa wengi wenu kwa kuwa ni siku isiyoingiliana na ratiba ya kazi. Tumekuwa na shughuli mbalimbali tangu tarehe 7 Julai 2022 za kusherehekea siku hii ya Kiswahili na leo tunahitimisha shughuli hizo. Hivyo, ninapenda kuwashukuru kwa dhati kwa kuweza kutumia muda wenu mahsusi wa mapumziko kuja kujumuika nasi katika shughuli hii.
Nne, naomba kuwashukuru wadau na marafiki wote ambao mmeshiriki pamoja nasi kwa michango yenu ya hali na mali kuandaa na kufanikisha siku hii maalum na muhimu kwetu. Nasema asante sana na niwaombe muendelee na moyo huo hata siku zijazo.
Tano, naomba nitumie fursa hii pia, kuwapongeza washiriki wote wa shindano hili. Leo tupo hapa na kusikia namna watakavyotoa hotuba zao kwa Kiswahili. Hii ni ishara dhahiri ya mapenzi na hamasa kubwa waliyo nayo kwa lugha hii na pia kwa utamaduni wa kiswahili.
Na mwisho, japokuwa si kwa umuhimu, niwashukuru sana watumishi wenzangu katika ubalozi kwa maandalizi mazuri ya shughuli yetu hii na niwatie shime muendeleze kazi hii nzuri.
II. HISTORIA YA LUGHA YA KISWAHILI
Ndugu Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana,
Naomba kwa nukta hii mniruhusu kuelezea, japokuwa kwa ufupi historia ya Kiswahili na nafasi ya Kiswahili kama lugha ya Taifa la Tanzania na pia kuhusu heshima hii adhimu tuliyopewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kuichagua Siku Mahsusi ya Kiswahili Duniani.
Pengine mtapenda kujua kuwa uamuzi wa kuibua tarehe 7 Julai kuwa Siku ya Kiswahili duniani unatokana na historia yenyewe ya matumizi ya lugha ya Kiswahili nchini Tanzania.
Kimsingi, uamuzi huu wa UNESCO unaweza unaweza kuelezwa kuwa unatokana na hatua ya Chama Cha ‘Tanganyika African Union -TANU, chama kilichopigania uhuru wa Tanzania (ikiitwa Tanganyika), ilipoundwa mnamo tarehe 7 Julai, 1954 chini ya uongozi wa Baba wa Taifa Hatyati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kutangaza rasmi kuwa Kiswahili kitakuwa lugha rasmi ya kudai uhuru wetu ndani na nje ya mipaka yetu.
III. KISWAHILI NA UKOLONI
Ndugu Wageni Waalikwa; Mabibi na Mabwana,
Ukifuatilia historia yake kwa karibu, lugha ya Kiswahili ilianza kutumika katika Pwani ya Afrika ya Mashariki ikijumuisha maeneo ya Tanga, Mombasa, Lamu, Dar es Salaam, Unguja, Pemba, Kilwa, Mafia, Lindi na Mtwara na huko ndiko kulikozungumzwa Kiswahili takriban miaka 1,000 iliyopita.
Lugha hii ilitokana na mchanganyiko wa lugha ya Kiarabu na lugha mbali mbali za Kibantu. Neno “Swahili” ni neno la asili ya kiarabu “Sahil” lenye maana ya pwani; sawahil’’au sawāhilī’’ ni wingi wake ikimaanisha yote yanayohusiana na pwani, watu na utamaduni wa eneo la pwani.
Kwenye karne ya 13, Kiswahili kilianza kama lugha ya miji na bandari za biashara ya kimataifa kwenye pwani ya Afrika ya Mashariki kama vile; Kilwa na miji mingine kadhaa iliyoanzishwa na wafanyabiashara Waarabu na Waajemi waliokuja kufanya biashara kwenye pwani ya Afrika Mashariki.
Mnamo mwaka 800 baada ya Kuzaliwa kwa Kristo, Kiswahili kilienea zaidi kwenye mji wa Unguja (uliopo kusini mwa Zanzibar ya sasa) ukiwa ni kitovu cha biashara ya kimataifa wakati huo.
Ndugu Wageni Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana,
Wakati wa kipindi cha Ukoloni, kwenye Karne ya 19 baada ya Kuzaliwa kwa Kristo, Tanganyika pamoja na nchi jirani za Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi ziliwekwa chini ya utawala wa kikoloni ambapo lugha ya kiswahili ilitumika kurahisisha mawasiliano kati ya wenyeji na wakoloni hao kutoka mataifa ya Ureno, Ujerumani na Uingereza.
Wakoloni hao walifika katika bandari za pwani ya Bahari ya Hindi na kuwatumia makarani, askari na watumishi kutoka maeneo ya pwani katika kujenga vituo vyao vya kiutawala. Aghalabu, kiswahili kilitumika sana katika kufanikisha shughuli za utawala huo wa kikoloni.
Pengine ni vema kueleza pia kuwa miaka hiyo ya ukoloni ilisababisha kupokelewa kwa maneno mapya kwenye lugha ya Kiswahili.
Mathalani, kufika kwa Wareno mnamo mwaka 1500 kulileta maneno kadhaa ya Kireno yaliyoingia kwenye lugha ya Kiswahili kama vile; "bendera" na "meza". Aidha, Kijerumani kiliacha maneno machache kama "shule" (Kijer. Schule) na "hela" (Kijer. Heller).
Wajerumani waliamua kutumia Kiswahili kama lugha ya utawala katika koloni lao la Afrika ya Mashariki ya Kijerumani mnamo miaka ya 1885 hadi 1918. Na wakati wa ukoloni wa Waingereza baada ya kuchukua Tanganyika kutoka kwa Wajerumani waliendelea kutumia Kiswahili kama lugha yao ya utawala.
IV. KISWAHILI NA HARAKATI ZA UHURU NA UKOMBOZI WA AFRIKA
Ndugu Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana,
Kama nilivyodokeza awali, wakati wa harakati za kudai uhuru wa Tanganyika, Baba wa Taifa na Rais wa Kwanza, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitumia lugha ya Kiswahili kama lugha kuu ya mawasiliano katika kuwahamasisha na kuleta umoja kwa wananchi wa Tanganyika kudai uhuru kutoka kwa wakoloni wa Waingereza.
Chama Cha TANU kilichoanzishwa tarehe 7 Julai, 1954 chini ya uongozi wa Hayati Mwalimu Nyerere kilitangaza rasmi kuwa Kiswahili kitakuwa lugha kuu ya kudai uhuru wa Tanganyika.
Aidha, baada ya kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika, Kiswahili kiliendelea kuwa kiunganisho kwa mataifa ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Jangwa la Sahara, kusini mwa Jangwa la Sahara katika harakati za kupigania uhuru katika mataifa hayo hata baada ya Tanganyika kupata uhuru wake mwaka 1961.
Ndugu Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana,
Hadi sasa, Kiswahili ni lugha rasmi ya Taifa na Serikali nchini Tanzania na katika shule za msingi hutumika kama lugha ya kufundishia ambapo, kwa shule za sekondari pamoja na vyuo vikuu kinatumika kama lugha mojawapo ya mawasiliano.
Aidha, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inatambua lugha ya Kiswahili kama lugha ya mawasiliano mapana (lingua franca) kwa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo ambapo, shughuli nyingi za kijamii, biashara, jeshi, michezo na sanaa kufanyika kwa kutumia lugha hii. Na hapa napenda kupongeza uamuzi wa busara wa hivi karibuni wa Serikali ya Uganda wa kujumuika na nchi wanachama wengine wa EAC kwa kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya nchi hiyo; na lugha ya kufundishia katika shule za msingi na sekondari.
Vilevile, kwenye Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Kiswahili kinatambulika kama lugha rasmi ya kazi ya Jumuiya ya SADC kuanzia mwaka 2018. Kukubalika kwa Kiswahili katika umoja huu, kunaifanya kuwa lugha ya nne katika Jumuiya hii.
Kadhalika, tarehe 15 Februari 2022, Umoja wa Afrika (AU) uliipitisha lugha ya Kiswahili, kuwa lugha rasmi ya kikazi ndani ya Umoja huo.
Pengine mtapenda kujua kuwa lugha ya Kiswahili kwa sasa inao wazungumzaji takriban watu milioni 200 walio ndani na nje ya Bara la Afrika. Idadi hiyo inakifanya Kiswahili kuwa lugha ya tatu kwa ukubwa Barani Afrika na moja ya lugha kumi zinazozungumzwa zaidi duaniani.
Kwa muktadha huo, Kiswahili kimekuwa ni mojawapo ya lugha rasmi nane zinazotambulika na Umoja wa Mataifa na kuepwa hadhi ya kuwa na Siku Maalum ya kuadhimishwa kimataifa. Lugha nyingine saba zilizopewa hadhi ya kuadhimishwa kimataifa ni; Kiingereza (23 Aprili); Kifaransa (20 Machi); Kichina (20 Aprili); Kiarabu (18 Disemba); Kireno (05 Mei); Kirusi (06 Juni) na Kispaniola (23 Aprili).
Ndugu Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana,
Pamoja na kwamba Kiswahili kinazungumzwa sana Afrika Mashariki, Afrika ya Kati, Afrika Magharibi, Kusini mwa Afrika, katika bara la Afrika na nje ya bara la Afrika, kinabakia kuwa na ya kipekee nchini Tanzania. Nchi yenye zaidi ya makabila 120 na kila kabila likiwa na lugha yake lakini imeweza kuzungumzwa na watanzania wote pasipo kujali asili zao.
Na kwa jambo hili kufanikiwa kwa kiasi hicho shukrani zimwendee Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na viongozi wengine waliofuatia baada yake kwa kujenga msingi mzuri na kukifikisha Kiswahili hapa kilipo leo hii.
Serikali ya Tanzania katika Awamu mbalimbali za uongozi imefanya jitihada mbalimbali za kukiwezesha Kiswahili kupiga hatua zaidi kitaifa na kimataifa. Miongoni mwa jitihada hizo ni kuanzisha vyombo mbalimbali vya kukisimamia na kukiendeleza Kiswahili.
Vyombo hivyo ni kama vile Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) sasa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI), Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA), Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni - Zanzibar (TAKILUKI), Chama cha Usanifu wa Kiswahili na Ushairi Tanzania (UKUTA) n.k.
Aidha, serikali ya Tanzania katika vipindi mbalimbali imekuwa ikitoa nyaraka na matamko mbalimbali ya kukipa hadhi Kiswahili na kuongeza matumizi yake kwa kuhamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili katika kutoa matokeo ya utafiti wa kisayansi na machapisho ya kitaaluma.
Pamoja na kuimarisha mafunzo ya lugha kwa kutoa programu maalumu ya lugha ya Kiswahili na lugha nyingine za kigeni kwa ajili ya kuzalisha wataalamu wa tafsiri na ukalimani wa Kiswahili kwenye viwango vya kimataifa.
Hivyo, ninapenda kutoa pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar; na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wao thabiti na kazi nzuri ya kuendeleza kukuza Lugha ya Kiswahili kwa kipindi hiki.
Tanzania inachukua hatua madhubuti sasa kukikuza Kiswahili na hata kuibidhaisha ndani ya nchi na duniani kote, kwa ujumla. Ili kufanikisha hili, Ubalozi unajipanga kuanzisha kituo cha kujifunzia lugha ya Kiswahili kwa wageni hapa nchini Japan kwa lengo la kujenga Diplomasia ya Uchumi kwa kutafuta soko la Kiswahili pamoja na kuitangaza lugha hiyo na utamaduni wake.
Na katika hili, nitaomba ushirikiano kutoka kwa marafiki zetu mliopo hapa leo na hata wale ambao hawakuweza kushiriki leo ili hatimaye tuweze kuanzisha Kituo hicho hapa Japan.
HITIMISHO
Ndugu Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana,
Naomba sasa kuhitimisha maneno haya machache kwa kuwashukuru, kwa mara nyingine, kwa kutupa fursa hii adhimu ya kujumuika pamoja kuadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani.
Mungu Ibariki Afrika,
Mungu Ibariki Tanzania,
Mungu Ibariki lugha yetu ya Kiswahili.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.