Mstahiki Meya wa Jiji la Nagai Shigeharu Uchiya,
Mstahiki Naibu Meyawa Jiji la Nagai Tamaki Saito,
Naibu Meya wa Jiji la Nagai,
Ndugu Toshihiro Takeda
Mkurugenzi Mtendaji Mwandamizi wa Mipango na Uratibu katika Jiji
la Nagai
Kanali Mstaafu Juma Ikangaa,
Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania unaoshiriki Nagai Marathon,
Ndugu Samson Ramadhani Nyonyi,
Kocha wa Timu ya Riadha ya Tanzania,
Bwana na Bib. Shimaoka,
Marafiki WakubwaRafiki wa Tanzania,
Watumishi wote wa Jiji la Nagai,
Ndugu Wanariadha kutoka Tanzania,
Ndugu Washiriki mliofika katika hafla hii,
Wageni waalikwa wote,
Ndugu Wanahabari,
Mabibi na Mabwana.
Jambo! Konnichi wa!
Ninaitwa Baraka Luvanda, Balozi wa Tanzania nchini Japan. Nilianza kuhudumu rasmi katika nafasi hii mwezi Januari mwaka 2022.
Hivyo, ifikapo mwishoni mwa mwaka huu nitakuwa nimetimiza miaka miwili.
Nianze hotuba yangu kwa kutoa shukrani kama ifuatavyo:
Mosi, nikushukuru sana Mstahiki Meya Uchiya kwa mwaliko wako kwangu na ujumbe nilioambatana nao kuja kujumuika katika Maadhimisho ya Mwaka huu ya Nagai Marathon.
Ninayo kila sababu ya kukushukuru. Kwa mwaliko wako huu, nimeweza kulipa deni langu kwako. Nilikuwa nadaiwa kufanya ziara hapa Nagai baada ya wewe Mstahiki Meya na ujumbe wako kututembelea Ubalozini Jijini Tokyo tarehe 18 Machi 2022. Asante sana Mstahiki Meya na watu wa Nagai.
Lakini pia ninakushukuru kwa kuniwezesha kukutana huku ugenini na ndugu zangu kutoka Tanzania. Ni fursa adhimu sana na ni furaha yangu kubwa kwamba Nagai mmeweza kufanikisha jumuiko hili kutokea.
Pili, naomba nitoe shukrani nyingi za Serikali ya Tanzania kwa Serikali ya Japan, kwa ujumla, na kwa Jiji la Nagai unaloliongoza kwa kukubali kuwa Mwenyeji wa Timu ya Wanariadha wa Tanzania katika Mashindano ya Olimpiki ya mwaka 2020 (2021) na baadaye kuendelea kuwa mfadhili wa miradi ya ushirikiano katika sekta ya michezo na masuala mengine ya kijamii na kiuchumi.
Nafurahi kumuona Bwana Erick Mfugale ambaye yuko hapa chini ya Mpango wa Kubadilishana Wataalamu wa Michezo (Sports Exchange Programme). Yeye ni mtu wa tatu kufuata baada ya Bwana Bahati Rogers, Bw. Charles Maguzu na Patrick Madinda waliokuwa wamemtangulia. Ni matamanio yangu kuona ushirikiano huu unadumu kwa muda mrefu kwa manufaa pande hizo mbili.
Tatu, Mstahiki Meya naomba nitoe pongezi nyingi kwako kwa kuwezesha haya yote niliyoyataja kufanikiwa kwa kiwango hicho kikubwa. Ninatambua mchango wako wewe binafsi lakini pia wa taasisi unayoiongoza. Pongezi nyingi sana kwenu nyote. Tunaona manufaa mengi ya ushirikiano huu na tunatambua mipango mingi mizuri iliyopo siku zijazo.
Mstahiki Meya, ninaomba pia nitumie fursa hii kuwapongeza sana Bwana Tsuyoshi Shimaoka na BibiYumiko Shimaoka kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kuimarisha kwa vitendo mahusiano ya Tanzania na Japan. Pongezi nyingi kwenu na niwatie shime muendelee na moyo huo huo.
Mwisho, lakini sio kwa umuhimu, naomba kwa nitoe shukrani zangu za dhati kwako Meya na Uongozi wote wa Jiji la Nagai kwa ukarimu wenu na mapokezi mazuri ya ujumbe wote wa Tanzania na mimi mwenyewe; na kwa maandalizi mazuri ya Mashindano ya mwaka huu.
Aidha, nawashukuru sana wadau na marafiki wote ambao mmeshiriki katika kuhakikisha mafanikio ya mashindano haya pamoja na ufadhili na uratibu wa kuileta Timu ya Riadha ya Tanzania na ujumbe wake kushiriki katika mashindano haya.
Mashindano haya yana umuhimu mkubwa katika kukuza vipaji kwa wanamichezo wa Tanzania pamoja na kudumisha uhusiano mzuri uliopo wa kati ya nchi zetu mbili.
Na pengine niwakaribishe sana ndugu zangu wanariadha kutoka Tanzania. Baadhi yenu ni wakongwe na wengine ni wageni. Nyote mjisikie mko nyumbani.
Tunaona fahari kubwa kwa ujio wenu na kwa kweli mtambue kuwa ninyi sio wakimbiaji tu bali ni Mabalozi wa Taifa letu kwa kuwa mnaitambulisha na kuitangaza vema Tanzania sehemu nyingi duniani kupitia michezo.
Tambueni kuwa kwa kila hatua mnayokimbia mnaonesha mazuri, utofauti na uthabiti wa nchi yetu katika medani za kimataifa.
Riadha ni mchezo unaohitaji kujitolea, uvumilivu, nidhamu na zaidi maandalizi. Na haya hayajapatwa kusemwa kwa msisitizo zaidi ya nukuu maarufu sana ya Kanali Mstaafu Juma Ikangaa ya, “The Will to win means nothing without the Will to prepare.”
Naamini mmejiandaa vizuri kutuletea sifa kwa mara nyingine tena na niwatie shime kuendelea na ari mliyonayo ya kuitangaza nchi yetu kupitia katika mashindano mbalimbali ya riadha.
Ndugu Washiriki,
Mabibi na Mabwana,
Nilipoambiwa nitazungumza mara baada ya Shujaa wetu tena Kanali Mstaafu wa Jeshi, Juma Ikangaa kuzungumza nilishikwa na dukuduku ama wasiwasi.
Na dukuduku hiyo ilikuwa kwa sababu za wazi kuwa pengine ningekosa cha kuongezea kwa yale atakayokuwa ameyadadavua kwa kina kutokana na ubobezi wake kwenye tasnia hii. Lakini pia kwa kuwa mimi siko ndani ya sekta yenyewe ya michezo.
Baada ya kusema hivyo, naomba sasa nizungumzie michezo kwa ujumla wake:
Michezo ina nguvu kubwa katika kuunganisha tamaduni, kujenga uhusiano na kudumisha mashirikiano kati ya mataifa.
Kwa mfano, ushiriki wa Timu ya Riadha ya Tanzania katika Nagai Marathon unadhihirisha urafiki na ushirikiano wa kudumu kati ya Tanzania na Japan, kwa ujumla, na Jiji la Nagai, kwa upekee.
Na hapa naomba nirejee shukrani za Serikali ya Tanzania kwa Jiji la Nagai kwa namna ambavyo mmeishirikisha Tanzania katika mashindano haya ya riadha na ya Besiboli. Na kama ilivyo kwa upande wa riadha, sasa hivi Tanzania inakuwa na mashindano ya kitaifa ya Besiboli ambayo imeanza kushirikisha na timu kutoka nje ya Tanzania.
Ndugu Washiriki,
Mabibi na Mabwana,
Tanzania ni nchi inayothamini michezo na kuipa kipaumbele sekta hii kwa kuwa imetoa ajira kwa vijana wengi pamoja na kuwa nyenzo muhimu ya kujipatia maendeleo hata kwa ngazi ya Taifa.
Kwa kutambua umuhimu huo, Serikali ya Tanzania kupitia Wizara inayosimamia masuala ya michezo inahakikisha sekta hiyo inasimamiwa na kuwezeshwa vizuri ili iweze kuchangia katika maendeleo katika maendeleo ya nchi.
Pamoja na kuwa na Wizara mahsusi kwa ajili ya michezo, Tanzania pia ina vyombo mbalimbali vya kusimamia sekta hii ikiwemo, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na Chuo cha Maendeleo ya Michezo cha Malya kinachotoa elimu ya stashahada ya michezo katika nyanja kuu tatu; Stashahada ya Uongozi na utawala katika michezo; Stashahada ya elimu ya michezo kwa michezo; Stashahada ya elimu ya ufundishaji michezo; zinazotolewa kwa muda wa miaka miwili.
Ndugu zangu wageni waalikwa,
Mabibi na mabwana,
Serikali pia inatekeleza kwa kutoa msukumo mkubwa kwa Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Michezo ya mwaka 1995.
Miongoni mwa malengo yake makubwa ni pamoja na kuhamasisha wananchi kushiriki michezo na mazoezi ya viungo vya mwili ili kuimarisha afya zao; kuhakikisha timu na wachezaji wetu wanashiriki kikamilifu katika mashindano na michezo ya kitaifa na kimataifa, kufanya utafiti wa Michezo ya Jadi kwa lengo la kuifufua na kuiendeleza, kuimarisha ushirikiano na mataifa mengine katika utoaji wa elimu kwa michezo na wanamichezo, kusimamia ujenzi wa miundombinu ya kisasa katika Sekta ya Michezo, kuimarisha Utawala bora katika michezo, kutoa Mafunzo ya wataalamu wa michezo, kupambana na Janga la UKIMWI katika michezo, na kuendeleza na kutambua vipaji vya vijana katika michezo kuanzia umri mdogo.
Aidha, Serikali inathamini mchango wa vijana na wanawake katika kuendeleza sekta hii nchini. Hivi sasa tumeshuhudia vijana wengi na wanawake wakishirikishwa katika maendeleo ya michezo ikiwemo, katika nafasi mbalimbali za uongozi katika michezo.
Pengine ni vema kutamka shukrani na pongezi nyingi za Serikali kwa Kanali Mstaafu Juma Ikangaa kwa kushrikiana na JICA kwa kujitolea kuwaendeleza wakimbiaji wa kike kupitia Mpango wa LADIES-FIRST TOURNAMENTS. Hongera sana, afande.
Kama ilivyoelezwa, kuwa Mstahiki Meya utakwenda Tanzania mwezi ujao kwa ajili ya kushuhudia mashindano yajayo ya LADIES-FIRST. Nikutakie safari njema.
Ndugu Washiriki,
Mabibi na Mabwana,
Naomba nisisitize kuwa Serikali pia inatambua kuwa maandalizi ya wachezaji mahiri hayana budi kuanza katika umri mdogo na kuwa endelevu.
Hivyo, imekuwa ikiwezesha mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA mashuleni, ili kusaidia kuibua mapema vipaji vipya na kuviendeleza.
Ndugu Zangu Washiriki,
Mabibi na Mabwana,
Ninapohitimisha hotuba hii, naomba kurejea shukrani zangu kwa Meya Uchiya na wananchi wa Jiji la Nagai kwa kujitolea kwenu pasipo kuyumba katika michezo; na kwa kuwakaribisha wanamichezo na ujumbe wa Tanzania kwa mikono miwili.
Kujitolea kwako katika michezo si tu kwamba kunadumisha umoja, bali pia kunatoa mwanga wa motisha kwa wanariadha na wapenda michezo.
Naomba nitumie fursa hii kutoa wito wa kudumisha ushirikiano huu kwa kuongeza wigo wa mashirikiano na Tanzania kwa michezo mingine ikiwemo, uogeleaji, mpira wa miguu, mpira wa kikapu na pete, ambayo, pia ina nafasi kubwa na kuwa na wapenzi wengi nchini.
Ninaamini ushirikiano huu ninaouomba utajumuisha maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na, kuwa na programu za kubadilishana wanamichezo, makocha, pamoja na matukio mengi zaidi ya michezo ikijumuisha, Nagai Marathon.
Rai yangu kwenu marafiki zetu Wa-Nagai wenye mitaji ni kuchangamkia zilizopo Tanzania kwa upande wa michezo hususan, katika kuendeleza na kujenga miundombinu ya michezo ikiwemo, ujenzi na ukarabati wa viwanja vya michezo na hata maeneo ya kufanyia mazoezi.
Ninaamini uwekezaji huo utawezesha nchi yetu kupanda katika viwango vya michezo kimataifa; na pia kwa vijana wetu kuweza kutumia fursa hiyo sio tu katika kuboresha maisha yao wakiwa Tanzania, bali hata kutambulika zaidi na kuonekana kimataifa katika vilabu mashuhuri vya michezo duniani au kutoka kwa wataalamu wa kimataifa katika fani mbalimbali za michezo.
Ndugu Washiriki,
Mabibi na Mabwana,
Naomba nihitimishe, kwa kutoa motisha kwetu sote kuwa siku ya kesho inapowadia, pale wanariadha wetu wanapofunga viatu vyao vya kukimbia na kujiandaa kushinda mbio hizi, ninawaomba wote tuungane kuwaunga mkono na kuwashangilia kwa moyo wote.
Tuungane sote kwa pamoja na kwa umoja kuchagiza ari ya ushindani na uthubutu kwa wanariadha wetu katika mashindano haya.
Na tunaposhuhudia wanariadha hawa shupavu wakivuka mipaka ya uvumilivu, tutafakari pia kuhusu malengo mapana ya maadhimisho haya ambayo ni kuimarisha afya ya mwili na akili, kukuza maelewano na kudumisha uhusiano miongoni mwa watu na mataifa mbalimbali.
Kwa kuwa mmenisikiliza kwa utulivu mkubwa, naomba nihitimishe kwa mchapo:
Marafiki wawili walikuwa wakimzungumzia jamaa mmoja: “Sitamwalika kamwe kwenye michapalo yangu”, mmoja alisema. “Safari iliyopita alifanya kitu sikukipenda kabisa.”
Alifanya nini?” “Alikuja.”
Mlitualika. Tunategemea mlimaanisha. Na hatuamini tutakuwa tumetenda lolote la kusababisha mtunyime mwaliko mwingine.
Mungu Ibariki Tanzania,
Mungu Ibariki Japan,
Mungu Ibariki Nagai,
Ahsanteni Sana kwa kunisikiliza.
Domo Arigato Gozaimashta.
Mstahiki Meya wa Jiji la Nagai Shigeharu Uchiya, akimkaribisha Mheshimiwa Balozi Baraka Luvanda, wakati wa Hafla ya Kuwakaribisha Wanariadha wa Tanzania kwenye Mashindano ya Nagai Marathon 2023, iliyofanyika tarehe 14 Oktoba 2023, jijini Nagai
Mheshimiwa Balozi Baraka Luvanda, akitoa hotuba wakati wa Hafla ya Kuwakaribisha Wanariadha wa Tanzania kwenye Mashindano ya Nagai Marathon 2023, iliyofanyika tarehe 14 Oktoba 2023, jijini Nagai
Kanali Mstaafu, Juma Ikangaa, Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania akitoa historia yake ya uanariadha, wakati wa Hafla ya Kuwakaribisha Wanariadha wa Tanzania kwenye Mashindano ya Nagai Marathon 2023, iliyofanyika tarehe 14 Oktoba 2023, jijini Nagai
Mstahiki Naibu Meya wa Jiji la Nagai, Tamaki Saito akifunga Hafla ya Kuwakaribisha Wanariadha wa Tanzania walioshiriki Nagai Marathon 2023, jijini Nagai
Sehemu ya wananchi wa Nagai waliohudhuria Hafla ya Kuwakaribisha Wanariadha wa Tanzania kwenye Mashindano ya Nagai Marathon 2023, iliyofanyika tarehe 14 Oktoba 2023, jijini Nagai
Balozi Luvanda pamoja na Wanariadha na Ujumbe wa Tanzania uliohudhuria Hafla ya Kuwakaribisha Wanariadha wa Tanzania kwenye Mashindano ya Nagai Marathon 2023, iliyofanyika tarehe 14 Oktoba 2023, jijini Nagai