Tanzania, kupitia Wizara ya Kilimo na Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini Japani, inaendelea kutangaza kahawa yake katika Maonesho ya Kimataifa ya Kahawa Maalumu (SCAJ 2026), yanayofanyika nchini Japani kuanzia tarehe 14 hadi 17 Oktoba 2026.
Maonesho hayo yanalenga kutangaza kahawa ya Tanzania, hususan aina za Arabika na Robusta, kupanua masoko ya kimataifa na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Japani.
Katika maonesho hayo, TCB imewezesha ushiriki wa kampuni tano za Tanzania ambazo ni Karagwe Estates Limited, Megnacio Company Limited, Lutefo Coffee Farm Limited, DRK General Merchants Ltd na Skyline Winner Company Ltd.
Kupitia ushiriki huo, kampuni za Tanzania zimefanya mazungumzo ya kibiashara (B2B) na kampuni mbalimbali za Japani, zikiwemo Ueshima Coffee Company Limited (UCC), Tully’s Coffee, Key Coffee, S. Ishimitsu & Company Limited na Marubeni Corporation, kwa lengo la kutafuta wanunuzi wapya na kupanua fursa za biashara.
Aidha, wageni waliotembelea banda la Tanzania wamepata fursa ya kuonja kahawa ya Tanzania, maarufu nchini Japani kama Kilimanjaro Coffee, na kueleza kuridhishwa na ubora na ladha yake.
Ushiriki huu ni sehemu ya utekelezaji wa diplomasia ya uchumi na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayosisitiza upanuzi wa masoko ya nje, uongezaji thamani wa mazao na kuimarisha mchango wa kilimo katika uchumi wa Taifa.
KAHAWA YA TANZANIA, FAHARI YA TAIFA!
Pichani: Balozi wa Tanzania nchini Japani, Mhe. Anderson Mutatembwa, akiwa na wawakilishi wa TCB, Bw. Rogatus Meela na Bi. Naishoki Lucumay, Maafisa wa Ubalozi na wawakilishi wa kampuni za Tanzania zinazoshiriki SCAJ 2026. Baadhi ya picha zikionyesha mikutano ya biashara iliyofanyika wakati wa maonesho hayo.
#SCAJ2026 #TanzaniaCoffee #KilimanjaroCoffee #EconomicDiplomacy #TanzaniaJapan



