Tarehe 9 Agosti 2026, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Japan, Mhe. Anderson Mutatembwa, alishiriki katika maadhimisho ya miaka 81 ya kumbukumbu ya shambulio la bomu la nyuklia lililotokea tarehe 9 Agosti 1945 katika Jiji la Nagasaki, nchini Japan. Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na Waziri Mkuu wa Japan, Mhe. Sanae Takaichi, viongozi mbalimbali wa ngazi za juu wa Japan, mabalozi 98 pamoja na manusura wa shambulio hilo (Hibakusha).

Shambulio hilo lilitokea tarehe 9 Agosti 1945, saa 11:02 asubuhi kwa saa za Japan, wakati bomu la nyuklia lililopewa jina “Fat Man” lilipolipuliwa katika anga la Bonde la Urakami, Jiji la Nagasaki, takribani mita 500 juu ya eneo la mlipuko (hypocenter). Bomu hilo lilikuwa na nguvu ya takribani kilotoni 21, sawa na nguvu ya mlipuko wa takribani tani 21,000,000 za TNT.

Kokura ndiyo ilikuwa mji uliolengwa awali. Hata hivyo, kutokana na mawingu na moshi uliokuwa umefunika anga la Kokura, eneo lililolengwa halikuonekana vizuri, hivyo ndege ilielekea Nagasaki ambako bomu lililipuliwa.

Kwa mujibu wa takwimu rasmi za Jiji la Nagasaki, hadi mwisho wa mwezi Desemba 1945, watu 73,884 walifariki na 74,909 walijeruhiwa kutokana na shambulio hilo. Aidha, kufikia 9 Agosti 2026, Daftari rasmi la Waliokufa kutokana na Bomu la Atomiki la Nagasaki lilikuwa na majina 204,708.

Viongozi wote waliozungumza katika maadhimisho hayo, wakiongozwa na Waziri Mkuu wa Japan, Mhe. Sanae Takaichi, walisisitiza umuhimu wa kudumisha amani duniani, kutatua migogoro kwa njia za amani na kuendelea na juhudi za kupiga marufuku utengenezaji na matumizi ya silaha za nyuklia, ili kuhakikisha kuwa janga lililolikumba Jiji la Nagasaki halijirudii tena popote duniani.