HOTUBA YA BALOZI BARAKA LUVANDA KATIKA MKUTANO MKUU WA PILI WA UMOJA WA WANAFUNZI WA TANZANIA WANAOSOMA NCHINI JAPAN (TSJ),

TAREHE 30 DESEMBA 2022, FUKUOKA, JAPAN

 

Ndugu Mwenyekiti wa TSJ Unayemaliza Awamu ya Uongozi;

Mwenyekiti Mpya wa TSJ;

Makamu Mwenyekiti wa TSJ;

Katibu wa TSJ Unayemaliza Awamu ya uongozi 

na Unayeanza Awamu

Nyingine ya uongozi;

Naibu Katibu wa TSJ;

Mwekahazina wa TSJ;

Ndugu wana-TSJ;

Wageni waalikwa;

Mabibi na mabwana.

 

Ninawasalimu kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Naomba nianze kwa kumshukuru sana  Mwenyezi Mungu kwa wingi wa rehema na baraka zake ambazo zimetuwezesha kukutana hapa leo. Ninaamini mnaungana nami katika kumrudishia Mungu sifa na utukufu kwa kutupendelea pumzi ya uhai hadi leo hii.

 

Pili, niruhusuni nitoe shukrani zangu za dhati kwa mwaliko wenu ambao umenipatia fursa ya kuungana nanyi leo kushiriki pamoja nanyi katika mkutano huu muhimu.  

 

Tatu, ni pongezi. Pongezi hizi nazielekeza kwa viongozi waliohitimisha awamu ya uongozi  kwa mafanikio makubwa lakini pia pongezi zangu kwa uongozi mpya wa jumuiya yetu kwa kuaminiwa katika nafasi zenu za uongozi na mwisho, lakini si kwa umuhimu niwapongeze sana ninyi nyote wana-TSJ kwa namna mlivyofanikisha kuunda umoja huu na kujenga mshikamano miongoni mwenu mkiwa huku ughaibuni.

 

Kama mjuavyo hata maandiko katika biblia (Zaburi 133:1) imebainishwa bayana kuwa, ninanukuu, “Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, ndugu wakae pamoja, kwa umoja.” Hongereni sana kwa kuliishi neno hili. 

 

Kipekee, ninawashukuru na kuwapongeza viongozi wanaohitimisha uongozi  wa jumuiya yetu. Mmefanya kazi nzuri sana.

 

Najua walikuwepo waliokuwa na shaka kuhusu kuanzishwa kwa jumuiya hii tunawaita “skeptics” ama “wet blankets” ambao walibeza na kuwakatisha tamaa. Kwamba umoja huu umehimili changamoto hizo kwa kipindi cha mwaka sasa ni jambo la kujivunia sana.

 

Hivyo, pamoja na kuwapongeza sana viongozi wapya kwa kuchaguliwa kushika nafasi za uongozi, niwatie shime katika  kuendeleza umoja wetu na kuuimarisha zaidi. 

 

Na labda niseme kuwa nimefarijika sana kuona angalau katika safu mpya ya uongozi kuna sura za zamani. Ni jambo zuri kuendeleza mazuri yaliyofanywa na kuendeleza dira ya jumuiya yetu.

 

Kwani pia ni ukweli usiopingika kuwa “ a new broom can sweep clean, but an old broom knows the corners.” Tulihitaji sana kuwa uwakilishi wa uongozi uliopita ili kunufaika na uzoefu wao ambao kama nilivyobainisha umefanya kazi nzuri sana.

 

 Ndugu zangu wana-TSJ,

Kwa kadri ninavyokumbuka, na kwa mujibu wa taarifa ya utendaji awamu ya uongozi uliopita imefanya mengi mazuri yanayopaswa kuenziwa.  

 

Kupitia jumuiya hii, mmeweza kujenga ushirikiano wa kusaidiana sio tu  katika masuala ya kielimu, bali pia katika masuala mengi ya kijamii, kwa ujumla wake. Mmekuwa mabalozi wazuri wa kuitangaza nchi yetu kwa kushiriki katika matukio mbali mbali  ambako mlipeperusha vema bendera ya Tanzania nchini Japan.

 

Kamwe siwezi kuelezea mafanikio yenu bila kutaja ushiriki wenu katika Mkutano wa Wana-diaspora na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa alipotembelea Japan mwezi Septemba mwaka huu. Hongereni sana kwa kazi nzuri ya kuhamasiha ushiriki katika mkutano ule muhimu na pia kwa mchango wa mawazo kwa Waziri Mkuu.

 

Aidha, siwezi kuacha kutaja kazi nzuri mliyoyafanya ya kuhakikisha watanzania wengi wanapata taarifa ya fursa za masomo kwa ufadhili zinazopatikana nchini Japan na ninaamini uongozi mpya utaendeleza jitihada hizi. 

 

Vile vile, siwezi kusahau mchango wenu wa hoja na mawazo mbali ambayo mmeyatoa kupitia machapisho mbali mbali, mahojiano kupitia vyombo vya Habari na semina mbalimbali mlizoshiriki yamewaongezea watanzania uelewa kuhusu Japan na manufaa mengi yaliyopo.  

 

Kadhalika, niwapongeze sana kwa kazi nzuri ya malezi kwa wanajumuiya wapya kila wanapoingia Japan. Mnaweza kudhani kuwa huo ni msaada kidogo. La hasha. Kwani tulishawahi kupata kisa cha mtanzania aliyeahirisha masomo yake  tena chini ya ufadhili kwa kushindwa kuhimili changamoto za ugenini. Niwaombe muendeleze utamaduni huo mzuri wenye manufaa kwa ndugu kwa jamii yetu.

 

Labda nirejee kutoa rai kama nilivyofanya mwaka jana kuwatakeni muendelee kuwa wageni wazuri nchini Japan na muendelee kutii  sheria za nchi mwenyeji wetu bila shuruti. Kwa kufanya hivyo, mtakuwa mmedumisha sifa nzuri ya Tanzania iliyozoeleka.

 

Mabibi na Mabwana,

Ninapokaribia kuhitimisha hotuba yangu hii fupi, naomba niseme kuwa Mkutano huu umenipa fursa adhimu ya kuonana nanyi kwa idadi kubwa kuliko ilivyokuwa mara ya kwanza mjini Tokyo mwezi Disemba mwaka jana. 

 

Na hivyo imenisaidia sana mimi na ninyi halikadhalika, katika kuweka sura kwenye majina niliyowahi kuyaona na kuyasikia kabla. Naamini tutaendeleza mawasiliano wakati wote tunapohitajiana. Kwa kawaida, milango ya ubalozi ninaosimamia iko wazi wakati wote na kwa aina yoyote ya huduma inayohitajika. Na tutaendelea kushirikiana nanyi bega kwa bega katika kutekeleza mipango ya jumuiya yetu mliojiwekea; kuendeleza mipango hiyo; kubuni mipango mipya kwa pamoja na kushirikiana kwa pamoja kuzitafutia ufumbuzi kwa pamoja changamoto mnazokabiliana nazo.

 

Na mwisho kabisa, kwa wale watakaokuwa wanahitimisha masomo yao siku zijazo na ambao pengine hatutapata fursa ya kuagana, niwatakie uhitimishaji mwema na safari njema ya kurejea nyumbani. 

 

Niwatakie nyote Kheri ya Mwaka Mpya wenye baraka tele.

 

Mungu Ibariki Afrika,

Mungu Ibariki Tanzania. 

Asanteni sana kwa kunisikiliza.