Tarehe 31 Januari 2023, Balozi wa Tanzania nchini Japan ambaye pia anawakilisha nchini New Zealand, Mheshimiwa Baraka Luvanda alikutana na kufanya mazungumzo pamoja na kula chakula cha jioni na Viongozi wa Jumuiya ya Watanzania waishio New Zealand (Tanzania New Zealand Association – TANZA). Viongozi hao waliambatana na baadhi ya wanachama wa Jumuiya hiyo, wakiwemo, Rais wa Jumuiya, Bw. Peter Mwelwa; Mshauri wa Jumuiya, Prof. Ernest Mudogo; na Katibu wa Jumuiya, Bi.Anna Mbalazi. 

Katika salamu zake, Balozi Luvanda alielezea furaha ya kukutana nao na kuwaeleza umuhimu wa Jumuiya za watanzania waishio nje ya nchi (Diaspora) na mtazamo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuwategemea kujenga uchumi wa nchi; pamoja na kushiriki katika mambo mbalimbali ikiwemo kuitangaza Tanzania katika nchi wanazoishi.

Katika mazungumzo, alitolea ufafanua wa masuala mbalimbali waliyotaka kuyafahamu likiwemo Uraia Pacha na kupatiwa Hadhi Maalum ambayo mchakato wake wameusikia kwa muda mrefu. Balozi Luvanda alieleza kuwa suala la uraia pacha lina changamoto zake ikiwemo kubadiri katiba na hivyo kwa sasa Serikali inaendelea na upatikanaji wa hadhi maalum. Aliendelea kueleza kuwa suala hilo lipo katika hatua nzuri na wategemee kupatikana hivi karibuni mchakato utakapokamilika.

Aidha, Balozi Luvanda aliwataarifu maendeleo ya utatuzi wa changamoto ya Pasi za kusafiria kwa watanzania ambao Pasi zao zimekwisha muda wa matumizi na mipango ya maandalizi ya Idara ya Uhamiaji kuja kuwahudumia hivi karibuni sambamba na waliopo nchini New Zealand. Viongozi hao walionyesha furaha yao kwa kukutana na Mheshimiwa Balozi na kueleza kuwa hatua hiyo itaimarisha mawasiliano baina yao na Ubalozi uliopo Tokyo nchini Japan.